Latest Posts

WAJUMBE IPU KUTOKA MATAIFA 16 WAGUSA MIRADI ARUMERU.

Ujumbe wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) kutoka mataifa 16 umetembelea miradi miwili ya maendeleo katika Wilaya ya Arumeru, ikiwemo mradi wa Zahanati ya Kiyoga na mradi wa umwagiliaji unaotekelezwa na vijana katika Kijiji cha Oloigeruno, Halmashauri ya Arusha DC.

‎Ujumbe huo umepokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Neema Lugangira, ambaye amepongeza hatua hiyo akisema inaendelea kuonyesha dhamira ya kushirikiana na Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi, hususan katika maeneo yenye mahitaji makubwa ya huduma za afya na kilimo.

‎

‎Lugangira amesema Arumeru ipo tayari kuendeleza ushirikiano na Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, ikiwemo UNICEF, WHO na WFP, pamoja na Mastercard Foundation na TAHA, huku akiomba miradi hiyo kuendelezwa katika maeneo mengine ya Arusha DC na Meru DC.

‎Kwa upande wake, Balozi na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa na Mashirika mengine ya Kimataifa, Hoyce Anderson Temu, amesema Tanzania imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano huo na kwamba tukio hilo linafungua fursa za ushirikiano na nchi mbalimbali duniani.

‎

‎Temu amesisitiza umuhimu wa kusimamia vizuri miradi inayotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, akieleza kuwa usimamizi mzuri ni muhimu katika kuhakikisha miradi hiyo inaleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wananchi.

‎Ziara hiyo imelenga kuwapa wajumbe hao fursa ya kujionea namna huduma za afya ya mama na mtoto zinavyotolewa katika Kituo cha Afya Kiyoga, ambacho kilipata ufadhili, pamoja na kujionea shughuli za vijana wanaojihusisha na kilimo cha umwagiliaji na uzalishaji wa mbogamboga.

‎

‎Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani unaendelea jijini Arusha, huku wajumbe kutoka mataifa mbalimbali wakiendelea kupata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali na kujionea utajiri wa urithi na utamaduni uliopo nchini Tanzania.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!