Rais Donald Trump, Jana Februari 2, 2026 alisema atachukua hatua za kisheria dhidi ya mtangazaji wa tuzo za Muziki za Grammy, Trevor Noah, kufuatia kauli ya mzaha aliyotoa akimhusisha Trump na marehemu Jeffrey Epstein, aliyekuwa na tuhuma za makosa ya unyanyasaji wa kingono.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa Tuzo za Grammy za 68, zilizofanyika Jumapili ya Februari 1, 2026 Noah alimpongeza msanii Billie Eilish kwa kushinda tuzo ya Wimbo Bora wa Mwaka kupitia wimbo wake Wildflower. Hata hivyo, katika mzaha wake, Noah alisema:
“Hiyo ni Grammy ambayo kila msanii anatamani kuipata, karibu kama vile Trump anavyotamani Greenland,” akirejelea kauli za awali za Trump kuhusu nia ya kutwaa eneo hilo
Noah aliendelea kwa kusema: “Ambalo linaeleweka, kwa sababu sasa Epstein hayupo, anahitaji kisiwa kipya cha kukaa na Bill Clinton.”

Kauli hiyo ilimkera Trump, ambaye alitumia mtandao wake wa Truth Social kushambulia hafla ya Grammy na mtangazaji wake. Trump alisema kuwa Tuzo za Grammy ni “mbaya zaidi na haziwezi kutazamwa,” kabla ya kumshambulia binafsi Trevor Noah.
Trump alikanusha madai hayo akisema: “Siwezi kuzungumza kwa niaba ya Bill, lakini mimi sijawahi kwenda Kisiwa cha Epstein, wala sehemu yoyote iliyo karibu. Kabla ya kauli hii ya uongo na ya kunidhalilisha iliyotolewa leo usiku, sijawahi hata kushutumiwa kufanya hivyo hata na vyombo vya habari vya uongo.”
Aidha, Trump alimuita Noah raia wa Afrika Kusini kuwa ni “mpotevu mkubwa” na kumtaka “arekebishe kauli yake.”
“Nitawatuma mawakili wangu kumshtaki huyu MC masikini, asiye na kipaji na mjinga… Jiandae Noah, nitakuwa na burudani kidogo na wewe,” aliongeza Trump.
Ikumbukwe kuwa Trump anatajwa kuwahi kuwa mshirika wa Epstein na kwa miezi kadhaa amekuwa akipinga kuachiliwa kwa nyaraka nyingi zinazomhusu mfanyabiashara huyo.
Trump pia amewahi kutoa maelezo yanayokinzana kuhusu sababu za kuvunjika kwa uhusiano wao.
Ijumaa iliyopita, zaidi ya nyaraka Milioni tatu zilichapishwa, zikitaja majina ya watu mashuhuri, akiwemo Trump, Elon Musk, Bill Gates na Bill Clinton