Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imetoa amri ya kufuta Vyama vyote vya Siasa nchini humo, ambavyo vilikuwa tayari vimesitishiwa shughuli zao tangu mapinduzi ya Kijeshi ya miaka minne iliyopita.
Uamuzi huo ulipitishwa na Baraza la Mawaziri jana Januari 29, 2026, ukiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kudhibiti upinzani wakati ikiendelea kukabiliana na mashambulizi ya makundi yenye uhusiano na al-Qaeda na ISIL.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Emile Zerbo, amesema hatua hiyo inalenga “kujenga upya taifa”, akidai kuwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ulikuwa umejaa ukiukwaji wa maadili na kushindwa kuleta mshikamano wa kijamii.
Kwa mujibu wa tathmini ya Serikali, kuongezeka kwa idadi ya Vyama vya siasa kulichochea migawanyiko na kudhoofisha mshikamano wa kitaifa. Kufuatia amri hiyo, mali zote za vyama vya Siasa zitachukuliwa na Serikali.
Kabla ya mapinduzi, Burkina Faso ilikuwa na zaidi ya Vyama vya siasa 100 vilivyosajiliwa, huku Vyama 15 vikiwa na uwakilishi Bungeni baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Hivi sasa nchi hiyo inaongozwa na Kapteni Ibrahim Traore, aliyechukua madaraka kupitia mapinduzi ya Septemba 2022, miezi minane baada ya mapinduzi mengine yaliyomuondoa Rais aliyechaguliwa kidemokrasia, Roch Marc Kabore.
Chini ya uongozi wa kijeshi, Burkina Faso imevunja mahusiano ya karibu na Ufaransa na kuimarisha ushirikiano wa kiusalama na Urusi.
Mwaka 2024, serikali iliamuru kusitishwa kwa tovuti na majukwaa ya kidijitali ya taasisi kama BBC, Voice of America na Human Rights Watch.
Aidha, Burkina Faso imeungana na Mali na Niger kuunda Muungano wa Nchi za Sahel (AES) kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kijeshi.