Latest Posts

TUME YA UCHAGUZI YAKANUSHA MADAI YA POLEPOLE

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imekanusha taarifa zinazodai kuwa mfumo wa uchaguzi unaotumika na Tume hiyo umeunganishwa na mfumo wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na chama cha siasa, hususan Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na madai kwamba zoezi la upigaji kura tayari limefanyika.

Mkurugenzi wa INEC, Ramadhan Kailima kupitia taarifa ya INEC ya Agosti 23, 2025, amesema taarifa hizo zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii ni za uongo na upotoshaji zenye lengo la kupotosha umma na kuibua taharuki.

“Taarifa hizo za uongo na upotoshaji zinaenezwa na mtu ambaye hana uelewa na ufahamu kuhusu mfumo wa uchaguzi. Daftari la Kudumu la Wapiga Kura halijaunganishwa na mfumo wowote wa Serikali au wa Taasisi binafsi kwa madhumuni ya upigaji kura”, amesema Kailima na kuongeza,

“Taarifa hizo za uongo na upotoshaji zinaenezwa na mtu ambaye hana uelewa na ufahamu kuhusu mfumo wa uchaguzi”.

Kailima amebainisha kuwa Tanzania haitumii mfumo wa kielektroniki katika kupiga kura, kuhesabu kura, au kutangaza matokeo. Badala yake, zoezi hilo hufanyika kwa kutumia utaratibu wa kawaida (manual).

“Ifahamike kuwa, Kitambulisho cha Taifa hakitumiki kupigia kura, bali Kadi ya mpiga kura pekee iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na kuhakikiwa ndiyo inayotumika wakati wa upigaji kura katika vituo vya kupigia kura”, amesisitiza.

Ameongeza kuwa vyama vya siasa vilishapewa Daftari la Wapiga Kura baada ya zoezi la uboreshaji kukamilika, na mawakala wa vyama watatumia daftari hilo kutambua wapiga kura siku ya uchaguzi.

Tume imewataka wananchi kupuuza taarifa hizo, ikisisitiza kuwa zinasambazwa na watu wasiokuwa na uelewa wa mfumo wa uchaguzi nchini.

Tume imewasihi wananchi na wadau wote wa uchaguzi kuupuza uongo na upotoshaji huo, na anayesambaza ana lengo la kuzua taharuki na upuuzwe kama wapotoshaji wengine.

Taarifa hii imetolewa kutokana na madai yaliyotolewa na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, usiku wa tarehe 22 Agosti 2025, ambapo alidai kuwa mifumo ya CCM imeunganishwa na ya INEC na NIDA kwa madhumuni ya kudhibiti matokeo ya uchaguzi.

Polepole alidai kuwa mifumo hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya na kupelekea vitendo vya kuomba namba za wapiga kura kutoka kwa watumishi wa umma.

Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unatarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!