Na Mwinyi Sadallah.
Katika wiki kadhaa zilizopita, Tanzania imekumbwa na hali ya wasiwasi baada ya baadhi ya watu kudaiwa kutekwa na kutoonekana mahali walipo, huku mjumbe mmoja wa sekretarieti ya CHADEMA akikutwa ameuawa. Hali hii inahitaji umakini mkubwa kutoka kwa viongozi na wananchi kwa jumla, ili kutafuta suluhisho la kudumu.
Katika utamaduni wa Taifa la Tanzania, kutekwa, kuteswa, na kujeruhiwa si mambo yanayokubalika. Hivyo, ni muhimu kwa watu wazima kukubaliana, kukaa chini, na kutafakari jinsi ya kuzuia matukio haya yasijirudie. Kwa miaka zaidi ya sitini ya kujitawala, Watanzania wamekuwa wakijenga taifa moja, na hakuna haja wala mantiki ya kugombania fito.
Kuendelea kutuhumiana kati ya upande wa utawala na upinzani kunachochea fikira chakavu zilizokosa mashiko ya kutosha.
Tatizo linapozuka na kuwa la kitaifa, viongozi katu hawapaswi kubabaika na kutaharuki, badala yake lazima wote wakae pamoja kama taifa ili kupatia utatuzi wake kwa kuhakikisha wahalifu wanapatikama katika kulinda usalama wa Taifa.
Ikiwa utawala utautuhumu upinzani kwa matukio haya au upinzani utaisema serikali au vyombo vya dola kuwa vinahusika, hizo ni fikra mfu zisizo na maana kamili. Majibu ya maswali haya hayawezi kupatikana kwa kunyoosheana vidole. Badala yake, inahitajika juhudi za pamoja kutafuta suluhisho la kudumu na kuondoa kadhia hii nchini.
Katika siku za hivi karibuni, kongamano la ekaristi ya tano lililoandaliwa katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam lilikuwa na umuhimu mkubwa. Viongozi wa kisiasa walihudhuria kongamano hilo, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA bara, Tundu Antipas Lissu, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Katika kongomano hilo kulioneshwa nini maana ya usawa wa binadamu na umoja wa watu. Hakukuwa na  madaraja yaliowagawa waumini katika itikadi za vyama, nasaba wala kukaa kwa nasabu ya rangi za waumini.
Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Wa Kanisa Katoliki (TEC), Padri Dkt. Charles Kitima aliposimama na kuwasimamisha viongozi hao watatu, umma ulilipuka kwa shangwe na sauti za matumaini. Shangwe na kelele zote za waumini hao, hazikuwa za shangwe kama lile la mashabiki wa Simba, Yanga, Malindi au Pamba na Majimaji; bali zilkuwa sauti za kutuma ujumbe kwa jambo muhimu lifike katika jamii.
Hadi sasa, watu kadhaa wamedaiwa kutekwa na kutojulikana mahali walipo, na kila upande unadai mwingine kujua mahali walipo na kuwaunga na kuuawa kwa kiongozi wa CHADEMA, marehemu Ali Mohammed Kibao. Tuhuma zote hizo zitabaki kama hisia au kupiga ramli kwa mtindo wa bahati nasibu au kucheza tombola.
Waswahili wa kale husema ‘siku zote shaka huwa haishiki mwizi’. Kumeibuka matukio mengi kabla ya hivi karibuni ya watu kutekwa na baadhi yao kupigwa risasi na kuuawa. Tiba ya matatizo haya haiwezi kupatikana kwa majibishano kwenye majukwaa ya kisiasa, mitandao ya kijamii, mikutano ya hadhara, au maandamano bila kibali. Njia bora ni viongozi kukaa chini, kubadilishana mawazo kwa ushirikiano na wadau wengine, na kujadiliana kwa kina ili kupata majibu na suluhisho huku wenye ushahidi wa kina waeleze kinagaubaga.
Kuitisha maandamano hakutakuwa suluhisho la matatizo haya. Badala yake, maandamano yanaweza kuwa chanzo cha kupoteza amani, utulivu, na umoja. Tumeyaona matokeo ya maandamano katika nchi jirani, ambapo maandamano yanapopandwa na munkari, huleta vurugu, vifo, na majeruhi.
Viongozi wanapokubaliana kwa nia moja kujifungia na kujadili hali ya kisiasa na kiusalama, kila jambo litapata majibu na suluhisho. Kila kitu kinawezekana kufanyika, kukamilika, na kuzuia kurudiwa tena. Njia pekee ni wanasiasa kukubali kusimama pamoja kama walivyofanya kwenye kongamano la ekaristi.
Tanzania ndiyo nchi pekee kusini mwa Jangwa la Sahara yenye sifa ya watu wake kuwa wavumilivu, wasikivu, na wenye kupenda mapatano na maelewano. Ustawi wa amani ya Afrika unategemea sana amani, umoja, na utulivu wa ndani wa Tanzania. Itakuwa kituko kusikia Tanzania ikipoteza amani kwa kushindwa kuelewana hadi kufikia maandamano. Ikiwa Watanzania watafikia hatua ya kushindwa kuelewana, bara la Afrika litaona Tanzania kama nchi iliyokosa mfano katika ustawi wa amani, demokrasia, na utawala wa sheria. Tutafika kwa umoja na kazi.