Latest Posts

KATAMBI: “MADARAKA YANAUA WATU”, MAASKOFU, MASHEIKH OMBEENI NCHI, INAWINDWA

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amedai kuwa Tanzania inawindwa sana kutokana na rasilimali zake na madaraka, akilinganisha hali hiyo na ukoloni mamboleo na kuonya kuwa machafuko yanayosababishwa na rasilimali na madaraka duniani kote huathiri zaidi watu wasio na hatia kama akina mama, watoto, na walemavu.

Ametoa kauli hiyo siku ya ‎Jumanne wakati akimwakilisha Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel Nchimbi katika maadhimisho ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Kanisa la Elim Pentekoste katika hafla iliyofanyika wilayani Karatu mkoani Arusha ambapo pia iliadhimishwa miaka 40 ya Askofu Mkuu wa Kanisa hilo la Elim Pentekoste Tanzania, Peter Konki.

“Taifa letu kama ilivyo kwingine duniani linawindwa sana, linawindwa siyo kwa bahati mbaya, ni kwa sababu zilezile, sababu zilizowaleta wakoloni hapa ndizo hizohizo zinawarudisha kwa staili nyingine, rasilimali zinaua watu, uongo kweli? Leo watu wanapigana, wanauana kwasababu ya mali, uongo kweli? Madaraka yanaua watu, uongo kweli? Leo nchi duniani huko kote kila mtu anataka kuwa mbabe, nani nani! Wanapigana, wanaathiri watu wa kawaida- akina mama, watoto, watu wenye ulemavu, wazee na watu wenye umri mkubwa ambao hawawezi kukimbia hata kilomita tano”, ameeleza Katambi.

Katambi amewaomba maaskofu, masheikh, na wachungaji kuombea nchi ili kulinda amani na kutoichukulia amani hiyo kama mzaha, akionya kuwa machafuko yanaweza kuifanya nchi kuwa na wakimbizi.

 

“Nchi yetu hii tuna historia nzuri ya amani, tuna historia nzuri ya kuwalea wenzetu waliopata machafuko, wenye busara hujifunza kutokana na makosa ya wengine siyo tufanye makosa yetu tuseme tumejifunza kutokana na makosa, makosa ya wengine yalitupa mafunzo kwamba kumbe mnaweza mkachafua taifa mkawa wakimbizi kwenye taifa jingine na mkapoteza haki zenu zote. Kwahiyo hata leo ukiangalia waliobaki na vyeo vyao nadhani ni Mababa Askofu na Wachungaji lakini bado wanaitwa wakimbizi kwenye maeneo mbalimbali”, amesisitiza Katambi.

 

Ameongeza kuwa Watanzania wanapaswa kuwa na umoja, uzalendo na mshikamano ili kulinda maslahi ya taifa dhidi ya changamoto na ushawishi unaoweza kuhatarisha maendeleo na usalama wa nchi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!