Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan amebainisha kuwa serikali yake ya awamu ya sita imefanya vizuri kwenye utekelezaji wa huduma ya usambazaji wa maji safi na salama nchini, akisema dhamira yake ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na huduma hiyo ya uhakika ikiwa atapata ridhaa ya kuchaguliwa tena na wananchi.
Dkt. Samia ameyasema hayo leo Jumanne Septemba 09, 2025 akiwa wilayani Bahi mkoani Dodoma kwenye muendelezo wa kampeni zake mkoani humo, akibainisha kuwa kwa Wilaya hiyo kwasasa vijiji 56 kati ya vijiji 59 vinapata huduma ya maji safi na ya uhakika, akibainisha kutambua changamoto ya maji kwenye vijiji vya Mpamantwa na Ibinwa.
Aidha akizungumzia tija ya ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa mkoani Dodoma, Dkt. Samia amesema kujengwa kwa reli na kituo cha SGR Wilayani Bahi pamoja na ujenzi wa bandari kavu kutaibadilisha Bahi kwa kiasi kikubwa na hivyo kuvutia uwekezaji pamoja na biashara, suala ambalo litakuza fursa za ajira kwa vijana wa Bahi na mkoa wa Dodoma kwa ujumla.
Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya elimu kwa kujenga miundombinu bora, ikiwemo mabweni kwa watoto wa kike wilayani Bahi, mkoani Dodoma. Aamesema serikali yake imejipanga kuongeza uwekezaji kwenye elimu ili kuondoa changamoto zinazowakabili wanafunzi, hasa wasichana, na hivyo kuwawezesha kufikia ndoto zao za kielimu.
“Tumejenga shule 14 za msingi na kufanya jumla ya shule za msingi ndani ya Bahi kufika 86. Tumejenga tena shule 3 za sekondari na sasa zipo 25. Tunapanga pia kujenga mabweni kwa ajili ya watoto wa kike, kwa sababu tumeona mwenendo wao na mila zetu wakati mwingine zinawazuia. Tukiwajengea mabweni itawarahisishia masomo,” amesema Dkt. Samia.
Aidha, ameeleza kuwa tayari serikali imejenga Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Bahi ambacho kwa sasa kina wanafunzi 156 wanaosoma fani mbalimbali zikiwemo ujenzi, uungaji vyuma, ubunifu na ushonaji, kompyuta, ufundi umeme na magari.
Dkt. Samia amesema uwepo wa VETA Bahi utasaidia vijana kupata ujuzi wa moja kwa moja kwa ajili ya kujiajiri na kuajiriwa kutokana na nafasi ya kijiografia ya wilaya hiyo, ambayo ipo karibu na mji na kwenye njia kuu ya kitaifa.