Katika kuadhimisha miaka 10 ya klabu ya mazoezi ya Gombani (Gombani Fitness club), klabu hiyo kwa kushirikiana na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar (TAMWA-ZNZ) na Shirika la Bima la Zanzibar wameandaa bonanza la mchezo wa mazoezi lenye lengo la kuhamasisha ushiriki wa wanawake na wasichana katika mazoezi na michezo.
Kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Kamati ya maandalizi, Bonanza la Michezo na Mazoezi Pemba, bonanza hilo litakaloshirikisha michezo ya aina mbalimbali litafanyika kisiwani Pemba kuanzia tarehe 20 hadi 28, Julai 2024.
“Viongozi mbalimbali wa serikali na taasisi binafsi wanatarajiwa kushiriki siku ya Jumapili ya tarehe 28 ambayo ndio itakua kilele cha maadhimisho hayo kwa kuanza na matembezi kutoka Madungu na kumalizikia katika Uwanja wa Mpira wa Gombani, kuanzia saa 12:00 asubuhi” Imeeleza taarifa hiyo.
Jumla ya michezo mitatu itachezwa siku hiyo ikiwamo mazoezi ya viungo, mchezo wa magunia na mchezo wa kuvuta kamba ambayo jinsia zote zitashiriki kwa kuonesha vipaji na uwezo wao.
Katika shamrashamra za kuelekea kilele cha maadhimisho hayo waandaaji wa bonanza hilo watapita skuli na shehia mbalimbali kuhamasisha kuhusu usawa wa kijinsia katika mazoezi na michezo, pamoja na kuwafundisha wanafunzi jinsi ya kujikinga na ukatili wa kijinsia (GBV) kupitia michezo maalumu inayojulikana kama (S4D acitivities).
Aidha jumla ya washiriki 500 kutoka maeneo mbalimbali ya Unguja, Pemba na Tanga wanatarajiwa kushiriki katika maadhimisho hayo ambapo kauli mbiu ni ‘Wekeza katika mazoezi na michezo kwa jinsia zote’.
Aidha wanamichezo wamehamasishwa kujikatia Bima ya ajali kwa Wanakikundi (Group Personal Accident) ambayo itakuwa inawakinga dhidi ya maumivu ya mwili na vifo vitakavyosababishwa na ajali wakati wakiwa katika mazoezi na harakati zao za michezo za kila siku.
Aidha wanakamati wameeleza kuwa katika miaka 10 ya Gombani Fitness Club tangu kuanzishwa kwake, mafanikio kadhaa yamepatikana ikiwamo kuimarika kwa afya za wana klabu, hata hivyo bado kuna changamoto mbalimbali kama kutokuwepo miundombinu rafiki ya kufanyia mazoezi kisiwani Pemba hususani kwa wanawake, dhana potofu dhidi ya mazoezi ya viungo, na kukosekana kwa taarifa sahihi juu ya umuhimu wa mazoezi na michezo katika vyombo vya habari.
TAMWA ZNZ inatekeleza programu ya michezo kwa maendeleo yenye lengo la kukuza usawa wa kijinsia katika michezo ambayo inatekelezwa kwa pamoja na Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Kituo cha Mijadala kwa Vijana (CYD) kwa ushirikiano mkubwa na Taasisi ya Maendeleo ya kimataifa ya Ujerumani (GIZ).