Latest Posts

VIJANA ZAIDI YA 3,000 WANUFAIKA NA MITAJI NA MAFUNZO KUTOKA SERIKALINI

Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana imeendelea kuweka mkazo katika kuwawezesha vijana wanaojishughulisha na shughuli za ujasiriamali kwa kuwapatia mitaji nafuu na mafunzo ya stadi za kazi. Katika mwaka huu wa fedha, kiasi cha shilingi bilioni 3.1 kimetolewa kufadhili miradi 141 ya vijana, sambamba na kutoa mafunzo kwa vijana zaidi ya 3,000 nchi nzima.

Akizungumza katika Kongamano la 9 la Ununuzi wa Umma (PPRA) lililofanyika mkoani Arusha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, alisema kuwa jitihada hizo ni sehemu ya Programu ya Taifa ya Ukuzaji Ujuzi. Kupitia programu hiyo, vijana wengi wameweza kurasimisha ujuzi walioupata nje ya mfumo rasmi wa elimu, hatua inayowasaidia kuingia rasmi katika soko la ajira na biashara.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA) Denis Simba amebainisha kuwa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 ni shilingi trilioni 56.5, ambapo kati ya asilimia 60 hadi 70 ya fedha hizo zitatumika kwenye ununuzi wa umma. Alisisitiza kuwa taasisi zote za umma zimeelekezwa kutenga asilimia 30 ya manunuzi kwa makundi maalum ikiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, ili kuongeza ajira, kukuza ujasiriamali, na kupanua wigo wa walipa kodi.

Kongamano hilo limeonesha dhamira ya dhati ya serikali kushirikiana na sekta binafsi katika kuinua uchumi kupitia ushiriki wa vijana na makundi maalum, huku teknolojia mpya kama NeST ikiongeza uwazi na ufanisi katika mifumo ya manunuzi na utoaji huduma serikalini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!