Latest Posts

VITISHO NA UTEKWAJI: ABDUL NONDO ASIMULIA TUKIO LILILOMKUMBA

Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa chama cha ACT Wazalendo Abdul Nondo ameeleza kuwa takribani watu sita waliovaa barakoa (Maski) zilizofunika eneo lote la nyuso zao walihusika kumkamata kwa nguvu akiwa katika eneo la Stendi ya Magufuli mkoani Dar es Salaam, kabla ya kutokomea naye.

Nondo ameeleza hayo katika mazungumzo ya simu na kituo cha habari cha DW Kiswahili akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan mkoani humo, ambapo amesema awali alidhani watu hao ni vibaka tu wa kawaida lakini alipoona hali imekuwa tofauti akajaribu kuomba msaada kwa wananchi waliokuwa jirani, hata hivyo juhudi hizo hazikuzaa matunda.

Amesimulia kuwa alifunikwa usoni, na kufungwa mikono yake kwa kamba na pingu kiasi cha kuumiza mishipa ya mikono yake, huku wakiendelea kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake na vitisho vya hapa na pale dhidi ya maisha yake vikishamiri.

“Neno kubwa ambalo walikuwa wakiniambia wakati wakiendelea kunipiga ni kwamba ‘wewe si chamdomo? (Mtu anayeongea sana), tutakuua wewe, wakawa wananitukana matusi makalimakali”, amesema Nondo.

Eneo la Coco Beach ndiko Nondo alipopatikana. Nondo amesimulia kuwa akiwa katika eneo hilo pasina kulitambua kutokana na kufunikwa uso wake, walimfungua kamba walizokuwa wamemfunga mikononi na kumfunua uso, katika hali ya kumuacha aendelee na maisha yake wakimpa onyo kukaa kimya katika harakati anazozifanya.

“Wakaniambia ukitoka hapa moja kwa moja nenda nyumbani, usipite sehemu yoyote, wala tusikusikie mahali popote, tusiisikie sauti yako kwenye chombo cha habari chochote, kama tuliweza kukukamata, na sasa hivi upo na sisi, tunaweza tukaamua hapa tukakuua, usipokaa kimya tutakukamata mara ya pili na tutakuua”, amesimulia Nondo.

Baada ya hapo alijikongoja eneo hilo la ufukwe wa bahari, kisha alipatiwa msaada na bodaboda waliompeleka ofisi ya chama ambapo kuanzia hapo alianza kufanyiwa hatua za kupatiwa matibabu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!