Katika kuhakikisha dunia inakuwa salama na binadamu kufaidika na uzalishaji wa chakula kutokana namazingira aliyopo,Mtaalam wa nyuki Dr.Kathrin Krausa kutoka shirika la Beetopia linalojishughulisha na uhifadhi wa kufanya tafiti na kutoa elimu kuhusu nyuki Mkoani Arusha, ameshauri binadamu kuanza kusikiiza changamoto za viumbe hai wanaosaidia katika uzalishaji hasa nyuki ili kuwe na uendelevu wa chakula.
Akizungumza na Jambo Media kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi zinavyo athiri ufugaji wa nyuki,amesema kuwa ni muda sahihi wa binadamu kutunza mazingira kwa kupanda miti rafiki itakayo wezesha nyuki na viumbe hai wengine wanao chavusha mazao kufanya kazi yao kwa faida yao na kwa binadamu mwenyewe.
“Nafikiri watu wengi wamesha hisi na kuona mabadiliko,wakulima wengi wanaogopa kwa kuhofia kupata mvua nyingi na baridi kali inayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi ni muda sahihi kwa wafugaji wa nyuki kuona namna ya kulinda mizinga na nyuki wao kwa kuwahamasisha kupanda miti ya kutosha inayoendana na mabadiliko ya tabianchi na inayo zalisha chakula kwa ndege na nyuki”Dr. Krausa
Krausa ameongeza kusema kuwa umefika muda wa kuwasikiliza ndega na nyuki kwa kuacha kufanya unyonyaji wa kuharibu mazingira badala yake kusikia wanasema nini kwa kuangalia afya na maisha yao na kuwasaidia katika kipindi hiki dunia inachopitia cha mabadiliko ya tabianchi.
Aidha amesema kuwa mabadiliko ya tabianchi yamesababisha mabadiliko kwa mimea kuchelewa au kuwahi kuchanua maua na kusababisha nyuki na ndege kukosa muda sahihi wa kupata chakula chao kwa wakati sahihi na mimea nayo kukosa kuchavushwa jambo ambalo ni hatari kwa mimea,ndege na nyuki.
“Ili kukabiliana na mabadiliko haya ni vema wafugaji wa nyuki na wakulima wengine kutizama mazingira kwa kupanda miti na mimea mingine ambayo ni afya na rafiki kwa ndege na nyuki ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi”Dr. Krausa
Ni wazi kuwa wanyama na wadudu wachavushaji wanakumbwa na changamoto kadhaa ambazo zina athiri mchango wao muhimu katika kilimo na mazingira ikiwemo kupoteza kwa makazi yao kutokana na ukataji miti,matumizi ya dawa za kilimo kwa kutumia viuatilifu na dawa za kuua wadudu,mabadiliko ya tabianchi ikiwemo kupanda kwa joto,ukame na mvua zisizo na mpangilio,uhamasishaji mdogo kuhusu umuhimu wa uchavushaji pamoja na uchafuzi wa mazingira.