Halmashauri 114 nchini zimeacha kugawa kingatiba za ugonjwa wa matende na mabusha kutokana na mafanikio ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo na hatimaye kwa sasa maambukizi mafia halmashauri hizo yamepungua na kufikia chini ya asilimia mbili.
Halmashauri hizo ni halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Lindi, Halmashauri za Wilaya ya Mtama, Pangani na Mikindani.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Januari 21, 2025 jijini Dar es Salaam na Kaimu Meneja wa Mpango wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP) kutoka Wizara ya Afya Dk. Faraja Lyamuya wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari na kuwajengea uelewa kuhusu magonjwa hayo.
Dk. Lyamuya ameeleza kuwa, imani potofu zilizopo katika jamii zinafifisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Amezitaja imani hizo kuwa ni pamoja na baadhi ya watu kuamini kwamba ugonjwa wa matende na mabusha ni wa urithi, unatokana na kulogwa na kuamini ni ugonjwa unaothiri ukanda wa Pwani pekee.
“Sio kweli kwamba ugonjwa wa matende na mabusha au ngiri maji, huambukizwa kwa kunywa maji ya madafu, wala si ugonjwa wa kulogwa, sio kweli kwamba ni ugonjwa unaothiri ukanda wa Pwani pekee bali maeneo yote yenye Mbu wenye vimelea watu wanaweza kupatwa na huu ugonjwa.
Akiongea katika mafunzo hayo, Afisa Mpango, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP) Dk. Lilian Ryatura amesema,
Halmashauri zilizokuwa na maambukizi ya juu ya zaidi ya asilimia 5 ya ugonjwa wa Trachoma (vikope) zilikuwa ni halmashauri 69 lakini baada ya kutoa kingatiba aina ya Zithromax, zimepungua hadi kufikia halmashauri tisa pekee.
Amezitaja halmashauri hizo kuwa ni, Longido, Ngorongoro, Monduli, Kiteto, Simanjiro, Kalambo, Mpwapwa, Kongwa na Chamwino huku akisisitiza kuwa ugonjwa huo hutibika kwa mtu kufanyiwa upasuaji mdogo wa kusawazisha kope.
Kwa upande wa ugonjwa Kichocho ambao ni miongoni mwa magonjwa ambayo yalikuwa hayapewi kipaumbele, Afisa Mpango Dk. Mohamed Nyati ameiasa jamii kumeza kingatiba ya Kichocho kila zinazotolewa kwenye jamii na shuleni kama njia kujikinga na ugonjwa huo.
Ameizitaja njia nyingine za kujikinga na ugonjwa huo kuwa ni pamoja na kutumia choo kw haja kubwa na ndogo, kuepuka kufua, kuogelea, au kuosha vyombo ndani ya maji yaliyotuama kama mabwawa, madimbwi na ziwani.
Ruth Mchomvu ni Afisa Mpango, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP) amesema, watu zaidi ya watu milioni 7.2 wanaoishi katika mikoa ya Morogoro, Ruvuma, Mbeya, Songwe, Tanga, Iringa, Njombe, Iringa na Dodoma wako hatarini kupata ugonjwa wa Usubi, ugonjwa ambao unaweza kutibika na kuzuilika
Lakini katika kuzuia hatari ya kupata ugonjwa huo, Mchomvu amesema ni muhimu kwa wananchi kumeza kingatiba za ugonjwa huo kila zinapotolewa kwenye jamii kaa kuwa dalili za ugonjwa huo huwa hazijtokezi mapema.
Kuhusu ugonjwa wa minyoo ya tumbo, Afisa Mpango Catherine Mahimbo amewaeleza waandishi wa habari kuwa, ugonjwa huo unaathiri watu wa rika zote wakiwemo watu wazima katika jamii na usipotibika mapema husababisha madhara lukuki.
Mahimbo ameyataja baadhi ya madhara kuwa ni pamoja na kupungua kwa damu, utapiamlo na kupungua uzito.
Madhara mengine ni udumavu wa akili na mwili kwa watoto, utumbo kujiunga, kujiziba na hatimaye kupasuka.
Mafunzo hayo ya siku moja yaliyoandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP) kwa waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, mbali na kuwajengea uelewa juu ya magonjwa hayo lakini pia ni moja ya mfululizo wa matukio kuelekea maadhimisho ya Siku ya Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 30 ya Mwezi Januari ambapo kulia mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu inasema “Tuungane. Tuchuke hatua. Tutokomeze Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele”.