Wadau wa masuala ya wanawake na uongozi wamevitaka vyama vya siasa nchini kuhakikisha vinawateua wanawake waliotia nia kugombea nafasi za uongozi kupitia uchaguzi wa ushindani, badala ya kuwaweka tu kwenye nafasi za viti maalum.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa Julai 27, 2025 na JUWAUZA, ZAFELA, PEGAO na TAMWA ZNZ kwa ushirikiano na Ubalozi wa Norway, wanawake wengi wamejitokeza kugombea nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani katika chaguzi za ndani ya vyama zinazoendelea kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Hata hivyo, kiwango hicho bado ni kidogo ikilinganishwa na idadi ya wanaume waliojitokeza.
Taarifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa Zanzibar inaonesha kuwa kati ya wanachama 1,640 waliorejesha fomu kugombea nafasi mbalimbali, wanawake ni 406 — sawa na asilimia 24.7. Kwa upande wa chama cha ACT-Wazalendo, kati ya wanachama 435 waliotia nia, wanawake ni 40 tu — sawa na asilimia 9.2.
“Mwaka 2020 Zanzibar ilipata wawakilishi wanawake wanane pekee katika Baraza la Wawakilishi, sawa na asilimia 16, na wabunge wanne sawa na asilimia 8 kupitia ushindani wa majimbo. Hili linaonesha bado kuna kazi kubwa ya kufanyika katika kuhakikisha usawa wa kijinsia kwenye uongozi wa kisiasa,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Wadau hao wamepongeza ujasiri wa wanawake waliojitokeza, lakini wakatoa rai kwa vikao vya uteuzi vya vyama kuhakikisha vinatoa nafasi halisi kwa wanawake kushindana katika majimbo na wadi badala ya kuwaacha kwenye hatua ya kuchukua fomu tu.
“Tunawasihi wajumbe wa vikao vya uteuzi wawapigie kura wanawake waliokidhi vigezo na kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika uongozi wa kisiasa. Wanawake ni sehemu muhimu ya maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ya Zanzibar,” wamesema wadau hao.
Wameongeza kuwa tafiti nyingi duniani zinaonesha wanawake ni viongozi waadilifu, wenye kujitoa na wanaojali zaidi maslahi ya familia na taifa kwa ujumla.
Pia wamekumbusha wajibu wa nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake (CEDAW), ikiwemo Tanzania, kuchukua hatua mahsusi za kuongeza uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya maamuzi.