Wadau wa maendeleo wamepongezwa kuendelea kuunga jitihada mbalimbali za kunyenyua mwanamke kiuchumi katika wilaya ya Mbeya Vijijini.
Hayo yamebainishwa na mwenyekiti wa halmashauri ya Mbeya Vijijini, Aida Haule wakati wa wiki ya maadhimisho ya wanawake duniani katika wilaya hiyo ambapo amesema wanawake ni jeshi kubwa hivyo amewaasa kuchangamkia fursa zinazotolewa na wadau pamoja na serikali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu ili kujikwamua kimaisha.

Aidha bi. Haule ameipongeza halmashauri hiyo kwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa wanawake hususani elimu juu ya ujasiliamali, uanzishaji wa viwanda vidogo vidogo na malezi bora kwa ustawi wa familia.
Akisoma risala kwa niaba ya mkuu wa divisheni ya maendeleo ya jamii wa halmashauri ya wilaya ya Mbeya vijijini Gift Kayunguya amesema madhumuni ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ni kuinua kiwango cha uelewa na ufahamu wa matatizo yanayowakabili wanawake duniani.
Maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliadhimishwa rasmi machi 08, 1857 nchini Marekani.