Rais wa Kenya William Ruto ametangaza awamu ya pili ya Baraza la Mawaziri tangu alipolivunja mnamo Julai 11 baada ya wiki kadhaa za maandamano makali dhidi ya serikali ambapo kati ya aliowateua wamo washirika wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye Ruto alimshinda katika uchaguzi wa 2022.
Katika hotuba yake akiwa katika Ikulu ya Nairobi siku ya Jumatano, Rais Ruto amemtangaza Kipchumba Murkomen kama mteule wa Waziri wa Masuala ya Vijana, Ubunifu na Michezo. Murkomen alikuwa waziri wa Uchukuzi katika Baraza la Mawaziri la zamani.
Wengine walioteuliwa katika nafasi ya uwaziri ni John Mbadi  ambaye ni mshirika wa Odinga (Wizara ya Fedha), Salim Mvurya (Uwekezaji), Rebecca Miano (Utalii), Opiyo Wandayi (Kawi na Petroli), Hassan Joho (Madini), Alfred Mutua (Kazi), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika), Justin Muturi (Utumishi wa Umma) na Stella Langat akiwa katika Wizara ya Jinsia.
Wateule wa hivi punde wanaungana na Duale, Tuya na wenzao wengine ambao Rais Ruto aliwatangaza Ijumaa iliyopita; Kithure Kindiki (Mambo ya Ndani), Alice Wahome (Ardhi), Julius Ogamba (Elimu), Andrew Karanja (Kilimo), Eric Muriithi Muuga (Maji), Davis Chirchir (Barabara na Uchukuzi), na Margaret Ndung’u (ICT).
Spika wa Bunge la Kitaifa la Kenya Moses Wetangula amesema wateule wote wa Baraza la Mawaziri watafanyiwa mchujo, wakiwemo wale walioteuliwa tena.