Latest Posts

WASIMAMIZI WA UCHAGUZI WATAKIWA KUEPUKA USWAHIBA WA KISIASA

Waratibu na wasimamizi wa uchaguzi wametakiwa kusimamia viapo, kutunza siri na kujitoa au kutokuwa mwanachama wa chama cha siasa katika kipindi chote cha uchaguzi ili kutimiza matakwa na masharti ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Akizungumza Julai 15, 2025 Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kuanzia Julai 15 hadi 17 yanayowakutanisha washiriki 119 kutoka mkoa wa Kilimanjaro na Tanga, yakilenga kuwajengea uwezo wa kusimamia uchaguzi mkuu ujao, Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi Dkt. Zakia Abubakar amewataka washiriki hao kusimamia viapo na kutunza siri kipindi chote cha uchaguzi ili shughuli ya uchaguzi ifanikiwe kama ilivyokusudiwa.

Amesema kuwa waratibu wa uchaguzi wa mikoa, wasimamizi wa uchaguzi, wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo, maafisa uchaguzi na maafisa manunuzi wanapatiwa mafunzo hayo baada ya kuteuliwa kwa mujibu wa sheria na tume ya uchaguzi kuwaridhia kutokana na utendaji wao wa uadilifu, uzalendo na uchapakazi.

Amewataka wanaosimamia uchaguzi kwa mara ya kwanza kujifunza kwa haraka na kupata uzoefu kupitia majadiliano ya pamoja, na wale wazoefu kutumia fursa hiyo kuongeza maarifa mapya na kubadilishana uzoefu na washiriki wengine.

Aidha amewataka kujiepusha kuwa vyanzo vya malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kwa kuzingatia ipasavyo kanuni, katiba, sheria na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na tume.

“Vishirikisheni vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili katika hatua zote kwa kuzingatia matakwa ya kikatiba, sheria, kanuni na maelekezo mbalimbali ya tume pamoja na wadau wa siasa ambao wanapaswa kushirikishwa kwa mujibu wa tume huru ya uchaguzi”, amesema Dkt.Zakia.

Mafunzo hayo yanaendeshwa nchini kote na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) yakilenga kuwajengea uwezo waratibu wapya na wa zamani juu ya namna ya kufanya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa njia ya haki na amani kwa ustawi wa Tanzania ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Kura Yako Haki Yako Jitokeze Kupiga Kura’.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!