Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limezindua kampeni maalum ya Shangwe la Sikukuu na TANAPA, Desemba 13, 2024, jijini Arusha. Kampeni hii inalenga kuhamasisha Watanzania na wageni kutembelea Hifadhi za Taifa wakati wa msimu wa Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya 2025.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia Maendeleo ya Biashara TANAPA, Jully Bede Lyimo, amesema TANAPA inasimamia hifadhi 21, ambazo ni miongoni mwa hifadhi bora barani Afrika na duniani.
“Hifadhi hizi zipo karibu kila mkoa wa Tanzania, na kutembelea vivutio hivi siyo tu kufurahia uasili wake, bali pia ni njia ya kuzitangaza hifadhi zetu kwa wageni,” amesema Kamishna Lyimo.
Aidha, amefafanua kuwa viingilio vinavyolipwa na Watanzania wanaotembelea hifadhi hizo vina mchango mkubwa katika pato la taifa, ambalo hutumika kujenga miundombinu kama barabara, viwanja vya ndege, hospitali, na shule.
Kwa zaidi ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa TANAPA, kampeni mbalimbali zimekuwa zikifanyika ili kuhimiza Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya utalii nchini. Kampeni ya mwaka huu inalenga kuwafikia watu kupitia ofisi, mitaa, na hata nyumba za makazi kwa lengo la kuongeza hamasa zaidi.
Kampeni hii ilizinduliwa kwa maandamano ya matembezi ya miguu yaliyochukua takribani masaa matatu, yakipita katika viunga vya Jiji la Arusha na kuhitimishwa kwenye viwanja vya Gymkhana. Shughuli hiyo iliwahusisha TANAPA, Chuo cha Taifa cha Utalii, wadau wa utalii, mchekeshaji maarufu Eliud Samwel, waandishi wa habari, na wananchi mbalimbali.