Na Josea Sinkala, Mbeya.
Jeshi la Polisi Mkoani Mbeya linawashikilia watuhumiwa watatu kwa tuhuma za mauaji katika kata ya Igurusi wilaya ya Mbarali mkoani humo kutokana na mgogoro wa mashamba baina ya familia mbili.
Akitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari, kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga, amewataja waliokamatwa kuwa ni Kuva Zengo (25), Lukeresha Mlawa (32) na Bulanda Mathias (25) wote wakazi wa Kijiji cha Luhanga wilayani Mbarali wakituhumiwa kwa mauaji ya watu wawili Iddi Wilbroad Mjengwa (38) mkazi wa Igurusi na Maige Jifaru (44) mkazi wa Isunura na kuwajeruhi watu wengine watano Wilayani humo (Mbarali).
Amesema kwamba mnamo Januari 10, 2025 majira ya saa kumi jioni huko katika Kitongoji cha Shitanda Kijiji na Kata ya Luhanga, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali ulitokea ugomvi baina ya familia mbili ya Rafael Ramadhani Mjengwa mwenye hati namba MBL/420 iliyotolewa mwaka 1987 dhidi ya familia ya Mzee aliyetajwa kwa jina la Malewa uliosababishwa na mgogoro wa ardhi ambalo ni shamba lenye ukubwa wa ekari 1050 ambapo familia ya Mzee Malewa pia wanadai shamba hilo ni la familia yao kwani wamekuwa wakilitumia kwa kilimo na kulisha mifugo kwa muda mrefu.
Ameeleza kuwa familia ya Mzee Rafael Ramadhani wakiwa wanaendelea na maandalizi ya kilimo katika shamba hilo, ghafla walishambuliwa na kundi la watu wapatao 15 wanaodaiwa kuwa ni wa Mzee Malewa na kusababisha watu wawili kufariki dunia na wengine watano kujeruhiwa.
Kutokana na tukio hilo, kamanda Kuzaga amesema ufuatiliaji umefanyika ambapo Januari 13, 2025 saa mbili usiku katika Kijiji na Kata ya Luhanga, Tarafa ya Ilongo, Wilaya ya Mbarali, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao ambao ni miongoni mwa watuhumiwa waliokuwa wakitafutwa kuhusiana na tukio hilo.
Ameeleza kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa jamii kuheshimu maamuzi ya mamlaka zilizopo ili kuepuka vitendo vya kujichukulia sheria mkononi na kusababisha madhara kwa watu wengine na endapo upande mmoja haujaridhishwa na maamuzi yaliyotolewa ni vyema kufuata taratibu za kisheria kwa kukata rufaa ili shauri lao liweze kusikilizwa upya.