Serikali imesema kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Tanzania ina jumla ya wazee 3,406,464 sawa na asilimia 6 ya Watanzania wote, ambapo wanaume ni 1,546,221 na wanawake ni 1,860,243.
Takwimu hizo zimetolewa leo na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, wakati akitoa taarifa kwa umma kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuelimisha na Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee, yanayofanyika kila Juni 15.
Mauaji Dhidi ya Wazee Yapungua, Serikali Yasema Mapambano Yanaendelea
Dkt. Gwajima amesema kuwa licha ya changamoto zinazoikumba jamii ya wazee, juhudi za Serikali na wadau mbalimbali zimeanza kuzaa matunda, ambapo kwa mujibu wa taarifa kutoka Jeshi la Polisi, mauaji ya wazee yamepungua kutoka 152 mwaka 2023 hadi 138 mwaka 2024.
“Jamii ina wajibu mkubwa wa kushiriki kikamilifu kuzuia na kukomesha ukatili dhidi ya wazee. Vitendo hivi vinawanyima wazee wetu haki ya kuishi kwa amani na furaha katika hatua hii ya mwisho ya maisha yao,” alisema Dkt. Gwajima.
Wito wa Kuchukua Hatua Mapema na Ushiriki wa Viongozi
Waziri Gwajima ameiasa jamii kuacha kauli na matendo ya ukatili dhidi ya wazee, akisisitiza kuwa taarifa za viashiria vya ukatili zinapaswa kutolewa mapema kabla madhara hayajatokea.
“Tunaomba jamii isisubiri hadi vitendo vya ukatili vitokee ndipo waanze kusema walikuwa wanahisi. Taarifa mapema zinaweza kuokoa maisha,” amesisitiza.
Aidha, amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha maadhimisho hayo yanaratibiwa kimkoa kwa kushirikiana na Mabaraza ya Wazee, na kwamba elimu ya haki, usalama na ustawi wa wazee itolewe kwa kina kwa wananchi.
Kaulimbiu ya Mwaka 2025: “Wazee ni Hazina kwa Taifa, Tuwalinde na Tuwatunze”
Tanzania huungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee kila mwaka ifikapo Juni 15. Kaulimbiu ya mwaka huu inalenga kuhamasisha jamii kutambua mchango wa wazee katika taifa na kuhakikisha wanatendewa haki.