Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeibuka kidedea katika Maonesho ya Wakulima Nane Nane Kanda ya Mashariki yaliyofanyika Mkoani Morogoro, baada ya kutwaa tuzo ya mshindi wa kwanza kwa Mkoa wa Dar es Salaam na kuibuka Mshindi wa Jumla wa Kanda ya Mashariki kwa mwaka 2026.
Katika maonesho hayo yaliyoshirikisha wadau wa sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, biashara, na teknolojia, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam (kupitia Wilaya ya Ilala) ilionesha ubunifu mkubwa katika kuwasilisha fursa mbalimbali za kiuchumi na mbinu za kilimo cha mjini.
Akizungumza wakati wa hafla ya ufungaji wa maonyesho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, ameeleza kuwa lengo la Serikali kupitia Nane Nane ni kuwawezesha wakulima wadogo na wakubwa kupata teknolojia, masoko, na mitaji.

Prof. Kabudi amezitaka mikoa yote kuhakikisha elimu na teknolojia zilizoonyeshwa Morogoro zinawafikia wananchi moja kwa moja.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali inaendelea kusimamia maelekezo yaliyotolewa wakati wa ufunguzi na Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, kuhakikisha maonyesho hayo yanakuwa endelevu na yanatumia teknolojia za kisasa.
Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi amewahimiza wananchi wanaojiajiri na wale wanaofanya kazi katika sekta binafsi wakiwemo wakulima na wafanyabiashara kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii kama vile NSSF ili kupata fursa ya bima ya afya na mafao ya ustaafu.