Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imeiagiza Wakala wa Vipimo (WMA) kuhakikisha mita za umeme zinahakikiwa kikamilifu kabla ya kufungwa kwa ajili ya matumizi, kwa kuzingatia sheria zilizopo ili kulinda haki za watumiaji.
Aidha, Kamati hiyo imeipongeza WMA kwa jitihada za uhakiki na ukaguzi wa vipimo mbalimbali, ikiwemo mita za maji, huku ikiitaka Wakala hiyo kuendelea kusimamia kwa ukaribu vipimo katika sekta ya ujenzi ili kupunguza malalamiko ya wananchi yanayotokana na bidhaa hizo.
Hayo yameelezwa leo Machi 14, 2026, na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Deodatus Mwanyika, wakati wa ziara ya kikazi katika Kituo cha WMA cha Uhakiki wa Vipimo Misugusugu mkoani Pwani kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo na kujionea shughuli za uhakiki wa vipimo zinavyotekelezwa kituoni hapo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, aliihakikishia Kamati kuwa wizara itatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa.
Alisisitiza kuwa azma ya Serikali ni kuhakikisha WMA inasimamia matumizi ya vipimo sahihi katika uzalishaji na uuzaji wa bidhaa mbalimbali, pamoja na Uhakiki wa mita za umeme na maji, ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Bw. Alban Kihulla, alisema kuwa ukaguzi na uhakiki wa vipimo una nafasi kubwa katika kuhakikisha haki na usawa baina ya pande mbili zinazofanya biashara.
Pia, aliwahimiza wananchi kuhakikisha wanatumia vipimo vilivyohakikiwa, huku akiwasihi watoa huduma kuzingatia uadilifu kwa kutoa huduma kupitia vipimo sahihi ili kuleta usawa na kuhakikisha bidhaa zinazonunuliwa zinaendana na thamani halisi ya fedha.
