Mwili wa Erick Mwangosi aliyekuwa dereva wa Pikipiki (Boda boda) katika kituo cha Ramadhani mjini Njombe,umekutwa ukiwa umetelekezwa kwenye pori lililopo kijiji cha Mtapa wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe
Akizungumza wakati wa mazishi katika makaburi yaliyopo mtaa wa Ramadhani Kelvin Ngulo ambaye ni mwenyekiti wa boda boda kanda ya Ramadhani anasema Erick alikodiwa na mteja tarehe sita na kushindwa kuonekana tangu tarehe hiyo jambo lililowafanya waanze kumtafuta mpaka mwili wake ulipopatikana kwenye pori ikiwa zimepita takribani siku tisa tangu alivyopotea.
“Ni jambo ambalo limetusikitisha sana kwa ndugu yetu kwa kuwa alikodiwa na watu ambao hatuwajui lakini kwa jitihada zetu tumeuona mwili sehemu inaitwa Mtapa akiwa ametupwa”amesema Ngulo
Kwa upande wao ndugu wa marehemu wamewashukuru wananchi kwa ushirikiano wa kumtafuta ndugu yao tangu tarehe sita ambapo wanasema kifo chake kimesababisha uchungu mkubwa kwa kuwa ameacha watoto watatu huku wakiomba jeshi la Polisi kuwabaini waliohusika na mauji ya ndugu yao waliyoyatekeleza na kupora Pikipiki.
Matukio ya wizi wa Piki piki mkoani Njombe yameendelea kuongezeka kwa kasi katika maeneo mbali mbali ya mkoa wa Njombe huku pia madereva wakiuawa na wengine wakijeruhiwa ambapo mkuu wa Polisi wilaya ya Njombe (OCD) CP Masoud Kwileka ametoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano ili kuwakamata watumiwa wa vitendo hivyo.
“Jukumu letu ni kusimamia amani na usalama wa wananchi na pale linapotokea jambo kama hili huwa hatufurahi na kuhakikisha wahusika wanapatikana,nitoe rai kwa wananchi kwamba sisi sote tunajukumu la kuhakikisha maeneo yetu yanakuwa salama kwa hiyo tunatakiwa tushirikiane kuhakikisha wahusika wanapatikana” amesema CP Masoud Kwileka