Latest Posts

JAMII YA WAMAASAI YAAZIMIA KILA MTOTO KUPATA ELIMU WILAYA YA SIHA

Jamii ya wafugaji wa kabila la Wamaasai wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro, imeshauriwa kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ili kuweka msingi wa maendeleo kwa vizazi vyao.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Siha, Meijo Laizer, Januari 29, 2025, wakati wa hafla ya kumpongeza Mwenyekiti wa Kijiji cha Donyomuruwa kwa ushindi wake katika uchaguzi wa viongozi wa vijiji, mitaa, na vitongoji uliofanyika Novemba 28, 2024.

Laizer amesema kuwa wazazi wa jamii hiyo wanapaswa kuhakikisha watoto wao wanapata elimu sawa na watoto wa jamii nyingine ili kuleta maendeleo katika maeneo yao.

“Mimi ni Mmasai, baba yangu hakuwa na uwezo mkubwa wa kunisomesha, lakini alijitahidi, nami nikaweza kupata elimu. Sasa, kama sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii yangu, mimi na marafiki zangu kutoka nje ya nchi tutajenga shule ya sekondari katika kijiji cha Donyomuruwa,” alisema Laizer.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Donyomuruwa, Meshaki Laizer, amesema kuwa jamii ya wafugaji hao imekubaliana kuwa kila mtoto anayestahili kwenda shule lazima apelekwe, na mzazi atakayeshindwa kufanya hivyo atawajibishwa kwa mujibu wa makubaliano yao.

“Tumeshaafikiana kuwa watoto wote waende shule, na wazazi wachangie chakula shuleni. Kama mzazi atakaidi, sisi wenyewe tutachukua chakula hicho kwa mujibu wa makubaliano,” alisema Meshaki Laizer.

Aidha, Laigwanan Mkuu wa Jamii ya Wamaasai Tanzania, Isack Ole Kasongo Meijo, amewataka viongozi waliochaguliwa kutekeleza majukumu yao kwa kuhakikisha watoto wote wanapata elimu, hasa ikizingatiwa kuwa serikali inatoa elimu bure.

“Kwa sasa si rahisi mzazi kuacha kumpeleka mtoto shule. Ataishi kitongojini au kijijini wapi bila elimu? Elimu ni bure, watoto waende shule,” alisisitiza Laigwanan Kasongo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!