Uwekezaji bandarini chini ya uongozi wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan umeanza kuonesha matunda makubwa baada ya serikali ya Tanzania kuokoa kiasi cha Dola milioni 600 sawa na Shilingi trilioni 1.5 katika miezi minne tu tangu kuanza kwa mkataba na kampuni ya DP World.
Kupungua kwa gharama za usafirishaji wa mizigo kumetajwa kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi, hivyo kuiweka Tanzania katika nafasi ya kuwa kitovu cha biashara na lango kuu la kiuchumi Afrika Mashariki.
Miongoni mwa mambo yaliyosababisha uokoaji wa kiasi hicho ni kupungua kwa muda wa kusubiri kwa meli za mizigo ya kontena na RORO, ambazo sasa zinaweza kutia nanga mara tu zinapowasili, kuboresha muda wa mzunguko na kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa.
Pia Ubia wa Kistratejia kati ya Serikali ya Tanzania na DP World umepelekea MSC kuondoa gharama ya ziada ya dola 1,000 kwa kila kontena ikiokoa Tanzania takriban Dola milioni 600 kila mwaka.
Aidha uendeshaji wa kreni umeboreshwa na uzalishaji ukiongezeka kwa kasi kutoka Mei hadi Julai 2024, na bandari ya Dar es Salaam kufanikiwa kushughulikia meli yake kubwa zaidi ya kontena hadi sasa, huku uimarishwaji wa ushindani wa Kanda nao ukitajwa kuchochea maendeleo hayo.
Bandari ya Dar es Salaam sasa inalingana na Mombasa katika ushughulikiaji wa mizigo, ikiiimarisha Tanzania kama lango kuu la bahari linalopendwa zaidi katika Afrika Mashariki.
Maboresho hayo yanatafsiriwa kuwa ni gharama ndogo kwa wafanyabiashara na kasi ya usindikaji wa mizigo, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia.