Latest Posts

MBUNGE BUSANDA AIMARISHA ELIMU KWA KUGAWA ‘PRINTA NA MASHINE YA FOTOKOPI

Katika jitihada za kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika shule za Jimbo la Busanda, Mbunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais , TAMISEMI, Dkt. Jafari Rajabu Seif, amekabidhi mashine za uchapaji na unakili wa nyaraka (printer na photocopy machine) zenye thamani ya shilingi milioni 12 kwa baadhi ya shule za jimbo hilo.

Ugawaji wa vifaa hivyo ni sehemu ya awamu ya kwanza ya mpango unaolenga kuzipatia shule zote za Jimbo la Busanda mashine hizo, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi katika uchapaji wa mitihani, nyaraka za kiutawala na kazi nyingine za kitaaluma, huku ikipunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili walimu na wanafunzi.

Akizungumza kwa niaba ya Dkt. Jafari Rajabu Seif, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Busanda, Philipo Manuali, alisema mbunge huyo anatambua kuwa elimu ni msingi wa maendeleo, hivyo ameona ni muhimu kuweka mazingira bora yatakayorahisisha utoaji wa huduma za elimu.

Alisema mashine hizo zitasaidia shule kuchapisha mitihani na nyaraka mbalimbali kwa wakati, pamoja na kuondoa mzigo uliokuwa ukiwaangukia wazazi wa kuchangia fedha kwa ajili ya gharama za uchapaji.

Manuali alibainisha kuwa zoezi la ugawaji wa vifaa hivyo litaendelea kwa awamu mbalimbali hadi shule zote zilizopo katika Jimbo la Busanda zitakapofikiwa, huku utekelezaji wake ukiratibiwa na Ofisi ya Mbunge.

Baadhi ya walimu waliopokea vifaa hivyo walimshukuru Dkt. Jafari Rajabu Seif kwa msaada huo, wakieleza kuwa utarahisisha maandalizi ya mitihani, kazi za ofisi na shughuli nyingine za kila siku shuleni. Walisema hatua hiyo itaongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, jambo litakalochangia kuinua kiwango cha elimu katika jimbo hilo.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!