Sakata linalomkabili mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Melkisedeki Kaijage, limechukua mwelekeo mpya baada ya Upande wa Mashtaka kubadilisha mashtaka yake na kumpa mashtaka ya ugaidi, chombo cha habari cha The Citizen kimeripoti.
Kaijage amekuwa mikononi mwa Jeshi la Polisi tangu tarehe 8 Julai 2026, alipokamatwa kwa mara ya kwanza kwa tuhuma za uchochezi wa maandamano ya umma ya tarehe 7 Julai, kosa ambalo awali alinyimwa dhamana.
Kutokana na hatua hiyo, Chama cha Wanataaluma cha Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA) kiliwasilisha maombi mahakamani kuomba apewe dhamana, ambapo shauri hilo lilisikilizwa Jumanne, tarehe 21 Julai 2026. Baada ya usikilizwaji huo, Mahakama ilitoa miongozo iliyomwezesha Mhadhiri Kaijage kukidhi vigezo vya kupata dhamana.
Hata hivyo, wakati mawakili wa utetezi na viongozi wa UDOMASA wakiwa katika mchakato wa kutekeleza amri hiyo ya mahakama ili kumtoa nje kwa dhamana, hati yake ya mashtaka ilibadilishwa na kusomewa mashtaka mapya.
Mwenyekiti wa UDOMASA, Dkt. Gerald Shija, amethibitisha kuwa mhadhiri huyo sasa anakabiliwa na kosa la ugaidi ambalo halina dhamana kisheria na tayari amehamishwa kutoka mahabusu ya polisi na kupelekwa katika Gereza Kuu la Isanga mjini Dodoma.