Latest Posts

SERIKALI YALIPA BILIONI 1.68 KWA WAKAZI WA BUHINGU, KIGOMA KUPISHA HIFADHI YA MAHALE

Serikali imelipa fidia ya kiasi cha Shilingi Bilioni 1.68 kwa wakazi wanaoishi eneo lililokuwa Kitongoji cha Kabukuyungu na Mahasa, Kijiji cha Kalilani Kata ya Buhingu Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma kutokana na eneo hilo kuwa chini ya umiliki wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale.
Zoezi hilo limefanyika  ili kupisha uhifadhi wa Mazingira endelevu kwa ajili ya hifadhi ya wanyama ikiwemo mnyama jamii ya Sokwe, ambapo kwa hatua ya awali  jumla ya kaya 205 kati ya 376 ambazo wakazi husika waliridhia kufanyiwa Tathmini ya mali zao, zimelipwa huku uongozi wa Serikali ya Mkoa ukitoa Rai kwa kaya ambazo hazijafanyiwa tathimini kuchukua hatua ili  kuepusha hasara ikiwemo kupoteza makazi  yao baada ya siku Sitini kuanzia Februari 25,2025 ambapo maeneo hayo yatarejeshwa rasmi kwenye umiliki wa Hifadhi hiyo.
Zoezi la ulipaji wa fidia, limeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, huku akitoa wito  jamii mkoani humo kuendelea kulinda Mazingira na viumbehai ikiwemo wanyamapori katika maeneo ya hifadhi ili kudumisha urithi huo wa Asili  kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.
Amesema wakazi wanapaswa kutambua umuhimu wa kulinda rasilimali za nchi ikiwemo wanyama aina ya Sokwe, ambao wanazidi kuadimika nchini  kutokana uharibifu wa Mazingira huku akisisitiza ulinzi wa  hifadhi ya Mahale na maeneo mengine tengefu mkoani Kigoma kwa ajili ya kutunza Mazingira na kudumisha Sekta ya Utalii ambayo inamchango mkubwa katika pato la Taifa.
Afisa Mhifadhi Mkuu Khalid Mgofi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale, ameipongeza Serikali kwa kuchukua hatua ya kuwabadilishia eneo la makazi wananchi hao sambamba na kutoa malipo ya fidia kwa kuwa kimsingi eneo hilo lilikuwa chini ya umiliki wa hifadhi tangu awali kabla ya kugeuzwa makazi.
Aidha baadhi ya Wananchi walionufaika na Mpango huo, wameupongeza uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kutekeleza zoezi hilo  kwa kuzingatia utu, jambo litakalowafanya  kutohangaika watakapohamia katika makazi mapya.
Aidha, wakazi hao wamesema, hatua hiyo imeondoa sintofahamu  iliyokuwa ikiwakabili na kusababisha kusimama kwa shughuli za Maendeleo ambapo mara baada ya malipo hayo wameahidi kutekeleza agizo hilo kwa kuhamia maeneo waliyotengewa ili kuendelea na shughuli za uzalishaji mali.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!