Latest Posts

ZAO LA UTALII WA FILAMU KUTIKISA TANZANIA

Katika kuendelea kuibua na kufaidi mazao mapya ya utalii nchini,Tanzania inaenda kukutanisha kazi zaidi ya 3000 za filamu kutoka Nchi zaidi ya 135 duniani kwaajili ya kutoa tuzo kwa washindi wa vipengele mbalimbali ambapo tayari filamu 100 zimechaguliwa kuwania tuzo.

Mkurugenzi wa tamasha la Kilimanjaro Film Festival Naamala Samson amesema kuwa   tamasha hilo litafanyika Mjini Moshi Mkoani Kilimanjaro  katika viwanja vya John Shule Park ,Karanga Magera kuanzia Julai 2 hadi 6,2025 ambapo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

“Tamashi hili linakusudiwa kuwa la kila mwaka, linalenga kukuza vipaji vya wasanii wa ndani na wa kimataifa, pamoja na kuimarisha utalii wa kitamaduni na ki-filamu kwa karne ya 21” alisema Naamala Samson

Amesema kuwa lengo kuu ni kutoa jukwaa kwa wasanii, watayarishaji wa filamu, na wawekezaji kubadilishana maarifa na kuunda mitandao ya ushirikiano ambapo tamasha hilo litajumuisha maonyesho ya filamu za Kiafrika na kimataifa, midahalo ya kisanaa, warsha za mafunzo kwa vijana na wanahabari wa filamu, pamoja na makongamano yatakayohusisha wadau wa utalii, sanaa na teknolojia.

“Tunataka Kilimanjaro Film Festival iwe sio tu tukio la burudani, bali pia chombo cha kukuza utalii kupitia filamu, huku tukitangaza uzuri wa Tanzania kwa macho ya kamera,tamasha hili linakuja katika kipindi ambapo utalii wa filamu (film tourism) unachukuliwa kuwa sekta yenye ukuaji wa kasi duniani,kupitia filamu, maeneo ya asili, historia, tamaduni na jamii za kiafrika zinapata nafasi ya kutangazwa duniani kote, hali inayochochea wageni kuitembelea Tanzania si kwa Mlima Kilimanjaro pekee, bali pia kwa historia na maisha halisi ya watu wake”aliongeza Naamala Samson

Tamasha hilo linatazamiwa kuibua fursa mpya za ajira, kuboresha mapato ya ndani kupitia wageni watakaoshiriki, na kukuza uwezo wa vijana katika sekta ya utayarishaji wa filamu na mawasiliano ya kisasa, pia itakuwa kichocheo cha kukuza lugha ya Kiswahili kimataifa kupitia filamu, sambamba na kuzalisha kazi bora zinazoweza kushindanishwa kwenye majukwaa makubwa ya filamu duniani.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!