Uandikishaji wa wanafunzi katika shule za msingi halmashauri ya Mbeya Vijijini kwa mwaka 2026 imefikia asilimia 76 ambapo wazazi wametakiwa kuendelea kujitokeza kupeleka Watoto shuleni kabla ya mwisho wa mwezi huu ili kufikia asilimia 100 ambayo wamejiwekea.

Rai hiyo imetolewa na mkuu wa wilaya ya Mbeya Solomon Itunda wakati akitoa salamu za serikali kwenye kikao cha robo ya pili ya kujadili taarifa ya mwaka 2025/2026 cha madiwani wa Halmashauri ya Mbeya Vijijini ambapo amewaasa kuendelea kuwahamasisha wazazi kuandikisha Watoto shule.

Itunda amewataka pia madiwani hao kuendelea kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo ya halmashauri hiyo ikiwepo pia usimamizi wa ukusanyaji wa mapato kwa mwaka huu.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Nsalala Festo Mbilike amesema uhamasishaji katika kata yake unaenda vizuri ambapo wazazi wamehamasika kwa kiasi kikubwa katika uandikishaji wa wanafunzi.
