Latest Posts

MWANASHERIA MKUU: TUJIIMARISHE NDANI MIGOGORO YETU ISITATULIWE NJE

Katika jitihada za kupunguza utegemezi wa mahakama na taasisi za kimataifa, Serikali ya Tanzania haina budi kuimarisha taasisi zake za ndani za usuluhishi wa migogoro ili iwe kituo kikuu na kinachopendekezwa kwa usuluhishi katika ukanda wa Afrika Mashariki na bara zima la Afrika.

Hayo yamebainishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari alipokuwa akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Nane wa Mwaka wa Taasisi ya Wasuluhishi Tanzania (TIArb) na Wiki ya Usuluhishi ya Dar es Salaam (DAR Arbitration Week) ya mwaka 2026 uliofanyika Julai 22, 2026. Amesisitiza kuwa ni wakati sasa kwa Tanzania kujenga uaminifu katika mifumo yake ya usuluhishi, badala ya kuendelea kupeleka migogoro kwenye mamlaka za kigeni.

“Badala ya kusafirisha migogoro nje ya nchi, tunapaswa kuendelea kuimarisha taasisi zetu za ndani ili Tanzania iwe chaguo la kwanza katika usuluhishi. Tunapaswa kujenga uaminifu huu siyo tu kwa migogoro yetu ya ndani, bali pia kwa migogoro inayoibuka Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla,” ameeleza Mwanasheria Mkuu huyo.

Aidha, amebainisha kuwa mabadiliko hayo yatajumuishwa katika zoezi linaloendelea sasa la kupitia na kuoanisha sheria za nchi ili ziendane na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.

Kwa upande wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Mustapher Mohamed Siyani amesema kuwa utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi na upatanishi unapaswa kutambuliwa kama sehemu muhimu ya mfumo wa utoaji haki nchini.

Katika hotuba aliyoisoma kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, George Masaju, Siyani ameeleza kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaielekeza Mahakama kukuza na kuimarisha utatuzi wa migogoro miongoni mwa wahusika wa migogoro kama ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo usuluhishi na upatanishi unapaswa kutazamwa kama mwendelezo wa jukumu la Mahakama katika utoaji wa haki ndani ya mfumo wa utawala wa sheria.

“Utoaji wa haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umepewa Mahakama. Hata hivyo, mamlaka hiyo haiwazuii wahusika wa mgogoro kutafuta haki kwa njia nyingine walizokubaliana, kama inavyoainishwa katika Ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inaielekeza Mahakama kukuza na kuimarisha utatuzi wa migogoro miongoni mwa watu wanaohusika katika migogoro hiyo,” amesisitiza Siyani.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!