Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, amesema kuwa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya usuluhishi na upatanishi, unapaswa kutambuliwa kama sehemu muhimu ya mfumo wa utoaji haki nchini.
Siyani ameyasema hayo tarehe 22 Julai, 2026, katika hotuba aliyoisoma kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, George Masaju wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Nane wa Mwaka wa Taasisi ya Wasuluhishi Tanzania (TIArb) na Wiki ya Usuluhishi ya Dar es Salaam (DAR Arbitration Week) ya mwaka 2026 uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaielekeza Mahakama
kukuza na kuimarisha utatuzi wa migogoro miongoni mwa wahusika wa migogoro kama ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo usuluhishi na upatanishi unapaswa kutazamwa kama mwendelezo wa jukumu la Mahakama katika utoaji wa haki ndani ya mfumo wa utawala wa sheria.
“Utoaji wa haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umepewa Mahakama. Hata hivyo, mamlaka hiyo haiwazuii wahusika wa mgogoro kutafuta haki kwa njia nyingine walizokubaliana, kama inavyoainishwa katika Ibara ya 107A(2)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inaielekeza Mahakama kukuza na kuimarisha utatuzi wa migogoro miongoni mwa watu wanaohusika katika migogoro hiyo,” amesisitiza Mhe. Siyani.

Amesema mifumo ya jadi ya utatuzi wa migogoro iliyokuwepo kabla ya ukoloni, iliyojengwa katika misingi ya maridhiano na maelewano, bado ina mchango mkubwa katika maendeleo ya mifumo ya kisasa ya utatuzi wa migogoro kwa njia ya Usuluhishi, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mifumo hiyo inaendana na mazingira ya Tanzania na inayokidhi viwango vya kimataifa.
“Uhalali wa mfumo wowote wa utatuzi wa migogoro hautegemei tu uhalali wake wa kisheria, bali pia kukubalika kwake na jamii pamoja na kuendana kwake na mila na utamaduni wa wananchi. Kwa hiyo, mustakabali wa mifumo ya Usuluhishi/upatanishi nchini Tanzania unapaswa kuwa shirikishi, ukichota mema kutoka katika mila na desturi mbalimbali huku ukizingatia misingi ya haki, kutopendelea upande wowote na utawala wa sheria,” amesema Jaji Kiongozi.
Kwa upande wake Rais wa Taasisi ya Wasuluhishi Tanzania (TIArb) Wakili Aderickson Njunwa, ameeleza kuwa, Taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1997, imebeba dhima kubwa ya kuisaidia jamii kutatua migogoro kwa njia ya upatanishi, kadhalika kukuza uwekezaji na kuimarisha uchumi endelevu.

Wakili Njunwa amefafanua kuwa miongoni mwa majukumu mengine ya (TIArb) ni kuhakikisha kuwa jamii ya Tanzania inapata elimu kuhusu maana ya usuluhishi na umuhimu wake kwa maendeleo endelevu pamoja na kuendeleza uwajibikaji kwa kujengeana uwezo na majukumu ya kitaasisi.