Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi, amechangia mifuko 92 ya sementi yenye thamani ya Shilingi milioni mbili (Sh2,000,000) kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Inglichini iliyopo Kijiji cha Malongo, Kata ya Miirare, Wilayani Rorya mkoani Mara.
Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi wa eneo hilo kuanza ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika shule hiyo mpya kupitia juhudi zao wakishirikiana na Mwalimu Mkuu. RC Mtambi ameamua kuunga mkono juhudi hizo, akivutiwa na utaratibu wa shule za msingi za Kata ya Miirare kuonyesha ufaulu mzuri mara kwa mara.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Afisa Elimu Msingi Kata ya Miirare, Mwalimu Kilunga Shallah, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa mchango huo na kueleza kuwa sementi hiyo itaharakisha ujenzi wa madarasa hayo mawili na kusaidia kuinua miundombinu ya shule hiyo mpya.