Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa amesema Mkoa wa Mbeya unaendelea kuimarika kiuchumi, ukiwa na fursa nyingi za uwekezaji katika sekta mbalimbali, na kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia mazingira mazuri yaliyopo kuwekeza.
Â
Akizungumza mkoani humo 23 Julai 2026 katika kikao maalumu na waandishi wa habari kilichoandaliwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kwa lengo la kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo mkoani Mbeya, Malisa amesema shughuli za uzalishaji zinazofanywa na wananchi hazitakuwa kikwazo kwa uwekezaji, bali zitaenda sambamba na maendeleo ya uwekezaji.

Â
Alibainisha kuwa Mkoa wa Mbeya una fursa nyingi katika sekta za kilimo, madini, mifugo, uvuvi, viwanda na maendeleo ya miundombinu, ambazo zinaweza kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi.
Â
Malisa pia ametaja maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji, ikiwemo Tanganyika Packers, Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Mbeya University of Science and Technology (MUST) pamoja na College of Business Education (CBE) – Kampasi ya Mbeya, akisisitiza kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na TISEZA kuhakikisha wawekezaji wanapata mazingira rafiki ya kuanzisha na kuendeleza miradi yao.
Â
Kwa upande wake, Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa TISEZA, Bw. Fedilis Obanga amesema ofisi ya TISEZA katika kanda hiyo imekuwa kiungo muhimu katika kuhamasisha uwekezaji, kutoa huduma za ushauri na kuwezesha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutekeleza miradi yao kwa ufanisi.

Amesema TISEZA imeendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali, sekta binafsi na wadau mbalimbali katika kutambua, kuendeleza na kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo, sambamba na kuwasaidia wawekezaji katika hatua zote za uwekezaji kuanzia utoaji wa taarifa, usajili wa miradi hadi utekelezaji wake.