Latest Posts

RAIS SAMIA: SERIKALI ITAENDELEZA MARIDHIANO YA KISIASA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendeleza maridhiano ya kisiasa kuelekea hatua za maboresho ya Katiba kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, Rais Dkt. Samia ameyasema hayo Julai 30, 2026, alipokutana na viongozi wa vyama 18 vya siasa nchini, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalihusu maridhiano, mageuzi ya kisiasa, uchumi, huduma za jamii, ajira, uwekezaji na ulinzi wa amani ya nchi. Akirejea hatua ya mchakato wa maridhiano visiwani Zanzibar, Rais Dkt. Samia amewaeleza viongozi hao hatua zilizofikiwa za maandalizi ya mchakato wa maridhiano kuelekea hatua zinazofuata za mapitio ya Katiba.

Amesisitiza kuwa hatua zote za mchakato huo zitafanyika kwa kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu zilizowekwa, kwa maslahi mapana ya Taifa, na kwamba Serikali itaendelea kukutana na viongozi wa vyama vya siasa kwa mazungumzo katika kipindi cha angalau mara tatu kwa kila mwaka.

Mkutano huo, uliowaleta pamoja wenyeviti, makamu wenyeviti, makatibu wakuu na viongozi wa jumuiya za vyama vya siasa nchini, ni wa pili wa aina hiyo kuitishwa na Rais Dkt. Samia tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Mkutano wa awali ulifanyika tarehe 31 Machi, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, ukiwakutanisha wagombea wa nafasi ya Rais na wagombea wenza kutoka vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Aidha, Rais amevitaka vyama vya siasa nchini kulinda amani, uhuru na maslahi ya nchi, akisisitiza kuwa ulinzi wa Tanzania ni wajibu wa pamoja baina ya Serikali, vyama vya siasa na wananchi wote.

Katika hatua nyingine, viongozi hao waliwasilisha maoni yao kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa wananchi katika nyanja za siasa, maendeleo ya jamii na uchumi. Serikali iliahidi kuendelea kuyapokea na kuyafanyia kazi mapendekezo hayo kupitia majukwaa stahiki ya majadiliano na mifumo rasmi ya maamuzi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!