Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imewasili rasmi Makao Makuu mkoani Morogoro tarehe 2 Septemba, 2026, ikiwa na tuzo mbili za Kimataifa za World Travel Awards (WTA) 2026 zilizotwaliwa na Hifadhi zake za Selous na Mpanga-Kipengere kufuatia hafla ya kutoa tuzo hizo iliyofanyika tarehe 28 Agosti, 2026, jijini Zanzibar.
Katika kinyang’anyiro hicho cha kimataifa, Hifadhi ya Selous imetwaa tuzo ya Kivutio Bora cha Utalii Afrika (Africa’s Leading Tourist Attraction 2026), huku Hifadhi ya Akiba ya Mpanga-Kipengere ikitwaa tuzo ya Eneo Bora la Mapumziko ya Harusi Afrika (Africa’s Leading Honeymoon Destination 2026), yakiwa ni mafanikio makubwa kwa TAWA katika ushiriki wake wa kwanza.
Akizungumza katika hafla ya mapokezi ya tuzo hizo, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mlage Y. Kabange, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kimkakati za kuitangaza nchi kupitia filamu za Tanzania: The Royal Tour na Amazing Tanzania, akieleza kuwa juhudi hizo zimeongeza mwonekano wa rasilimali za Tanzania duniani.
Kabange amebainisha kuwa matokeo ya ushindi huo yameanza kujitokeza mara moja, ambapo kampuni moja ya ndege kutoka Zanzibar tayari imeonyesha utayari wa kuanzisha safari za moja kwa moja kwenda Hifadhi ya Mpanga-Kipengere mara tu miundombinu itakapokamilika, jambo litakaloimarisha utalii, mapato, na ajira kwa jamii.

Akitumia fursa hiyo, Kabange amewakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika miundombinu ya malazi na huduma za utalii katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA, huku akitangaza mpango wa kuzipeleka hifadhi nyingine kama Makuyuni na Pande katika mashindano ya kimataifa siku za usoni.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Emmanuel B. Musamba, ameeleza kuwa tuzo hizo ni kura ya imani ya kimataifa kwa ubora wa hifadhi za Tanzania na ufanisi wa juhudi za uhifadhi endelevu.
Musamba amehitimisha kwa kusisitiza kuwa ushindi huo unaongeza wajibu kwa TAWA kuhakikisha ukuaji wa sekta ya utalii unakwenda sambamba na hifadhi endelevu ya mazingira na kutoa mchango mkubwa kwa uchumi wa taifa.

