Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amekataa katakata matumizi ya dhana ya “kesi za kisiasa” mahakamani, akisisitiza kuwa mahakama zinasimamia sheria na sio siasa, na kutoa onyo kuwa CCM haiwezi kuingilia uhuru wa mahakama kwa kufuta kesi zilizopo kwani kufanya hivyo ni kukigeuza chama tawala kuwa mahakama yenyewe.
Wasira amebainisha hayo leo Septemba 8, 2026, wakati akihutubia katika Mkutano wa Kitaifa wa Wadau wa Kutafakari Hali ya Siasa nchini unaofanyika mkoani Dar es Salaam.
“Mimi sielewi kesi za kisiasa zinavyofanana. Najua kesi ambayo iko mahakamani huwezi kuita ya kisiasa. Maana mahakama hizi hazikusomea siasa. Mahakama wamesomea sheria,” amesisitiza Wasira
Ameongeza kuwa mahakama ni chombo huru cha kutoa haki, na kwamba mtu yeyote anayefikishwa mbele ya sheria akiwa hana kosa, mahakama ikiridhika kuwa hana hatia itamwachia huru.
Wasira alishirikisha uzoefu wake binafsi wa kisheria ili kuonyesha uhalisia wa mahakama, akifichua kuwa amewahi kushtaki na kushtakiwa mara kadhaa katika maisha yake. Katika mnyukano huo wa kisheria, alieleza kuwa alifanikiwa kujinasua katika baadhi ya kesi, akashinda nyingine, na baadhi akashindwa, jambo linalothibitisha utendaji wa kawaida wa kimahakama.
Kuhusu hoja kuwa uhuru wa mahakama unahujumiwa pale viongozi wa mahakama na bunge wanapokutana na viongozi wa serikali kuu, Wasira amezima shutuma hizo kwa kueleza kuwa kukutana na kujadiliana kati ya mihimili ya dola ni jambo la kawaida na la afya. Amesema kuwa mihimili hii haipaswi kuishi kwa uadui au migogoro ya mara kwa mara
“Kunywa chai na Rais hakukupi haki ya wewe kwenda kuhukumu vibaya. Hiyo ni kawaida tu,” amesisitiza, akionesha kuwa mawasiliano hayo ya kijamii na kiitifaki kati ya Rais, Jaji Mkuu, au Spika hayamaanishi kuingiliwa kwa maamuzi huru ya kisheria ya mahakama.