Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamshikilia mtu mmoja, Conrad Agonza Kayoza, mwenye umri wa miaka 35, kwa tuhuma za kumshambulia kwa ngumi na mateke askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani(‘traffic’) katika eneo la Lugalo, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda hiyo SACP Muliro Jumanne Muliro imesema tukio hilo limetokea Septemba 8, 2026, majira ya saa 1:30 asubuhi katika Barabara ya Bagamoyo, wakati askari Polisi namba F.8886 SGT Andrew alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kikazi kwa kuwazuia kisheria madereva waliokuwa wakitumia pembezoni mwa barabara, maarufu kama ‘Service Road’, nje ya utaratibu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, mtuhumiwa alishuka kwenye gari aina ya Toyota RunX lenye namba T 455 EER baada ya kusimamishwa na kuanza kumshambulia askari huyo kwa ngumi na mateke. Baadaye wananchi waliokuwa eneo hilo walimshambulia mtuhumiwa, ambaye alipelekwa hospitalini kwa matibabu.
Polisi imesema baada ya mtuhumiwa kupata nafuu atahojiwa kwa kina na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. Aidha, Jeshi hilo limetoa onyo kali kwa mtu yeyote au kundi lolote linalowashambulia askari wakati wakitekeleza majukumu yao ya kisheria, likisisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua za kisheria.