Latest Posts

MASAUNI ATOA WITO KULINDA TABAKA LA OZONI

Na Vivian Ricardo,

Serikali imewataka Watanzania kuepuka kuingiza nchini gesi zilizopigwa marufuku pamoja na majokofu na viyoyozi vilivyotumika vinavyotumia kemikali zinazoharibu Tabaka la Ozoni, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kulinda mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, katika tamko lake kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni yanayofanyika Septemba 16 kila mwaka.

Screenshot

Masauni amesema Tabaka la Ozoni lina jukumu muhimu la kuchuja mionzi hatari ya jua kabla haijafika duniani, huku akionya kuwa uharibifu wake unaweza kuongeza hatari ya saratani ya ngozi, mtoto wa jicho na kudhoofisha kinga ya mwili.

Ameeleza kuwa baadhi ya kemikali zinazotumika katika majokofu, viyoyozi, vifaa vya kuzimia moto na shughuli nyingine za uzalishaji ndizo zinazochangia uharibifu wa Tabaka la Ozoni, hivyo matumizi ya kemikali rafiki kwa mazingira yanapaswa kupewa kipaumbele.

Amesema maadhimisho ya mwaka huu yanaadhimisha pia miaka 10 tangu kupitishwa kwa Marekebisho ya Kigali ya mwaka 2016, ambayo yanaimarisha juhudi za dunia za kupunguza matumizi ya kemikali zinazochangia ongezeko la joto duniani.

Masauni amewahimiza wananchi kununua bidhaa zenye alama ya “Ozone Friendly” au “Low Global Warming Potential”, kuepuka kutupa ovyo vifaa vya zamani vyenye kemikali hatari, na kushiriki kikamilifu katika juhudi za Serikali za kuhifadhi Tabaka la Ozoni kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!