Latest Posts

KUJIANDAA NA MVUA ZA EL-NINO NA KAMPENI KABAMBE YA USAFI WA MAZINGIRA, RC CHALAMILA ATOA MALEKEZO MAHUSUSI

   

SERIKALI ya Mkoa wa Dar es Salaam imetoa maelekezo mahususi kwa halmashauri zote mkoani humo yakilenga kujipanga kikamilifu kukabiliana na athari za mvua za El-Nino, huku ikitangaza kampeni kabambe ya kuurejesha mji katika hali ya usafi kufuatia kusuasua kwa usimamizi wa hivi karibuni.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amebainisha hayo Septemba 17, 2026 wakati wa mkutano wake na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na kueleza kuwa, serikali ya mkoa huo imekiri kuwepo kwa uzembe uliomfanya Rais Samia Suluhu Hassan kukosoa muonekano wa jiji hilo.

 

Ili kurekebisha hali hiyo, Chalamila amewapa wakandarasi na halmashauri muda wa miezi mitatu kupata vifaa vya kisasa na kuweka taa katika maeneo 50 ya msingi ili usafi ufanyike usiku badala ya mchana, sambamba na kuagiza kusafishwa kwa mifereji na mito mikubwa kama Mto Msimbazi ili kuzuia mafuriko.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuitisha kikao hicho na kusisitiza utayari wa wakuu wa wilaya zote kusimamia na kutekeleza maagizo yote yatokanayo na mkutano huo kwa asilimia mia moja.

Mpogolo ameongeza kuwa, ushirikiano wa karibu kati ya serikali na vyombo vya habari umekuwa chachu kubwa ya mafanikio katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na usimamizi wa mazingira jijini.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, akizungumza kwa niaba ya wahariri na waandishi wa habari, amepongeza jitihada hizo na kuahidi kuwa vyombo vya habari viko tayari kushirikiana bega kwa bega na serikali ya mkoa kuelimisha umma kuhusu mabadiliko ya utamaduni wa usafi, utenganishaji wa taka, na uondoaji wa biashara zisizo rasmi kando ya barabara.

Kwa upande wa usimamizi wa sheria za mazingira, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa  la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambaye pia ni Meneja wa NEMC Kanda ya Mashariki na Kaskazini (inayosimamia wilaya za Kinondoni, Ubungo na Kibaha), Glory Kombe, amethibitisha kuwa Baraza hilo litahakikisha sheria na miongozo yote ya hifadhi ya mazingira inazingatiwa kikamilifu ili kuzuia uchafuzi na maafa wakati wa mvua.

Kufuatia maelekezo hayo, Mkoa wa Dar es Salaam unawasihi wananchi wote kuacha tabia ya kutupa taka kwenye mifereji ya maji na kuwataka wale wanaoshi katika maeneo hatarishi ya mabondeni kuhama mara moja kabla ya mvua hizo kuanza ili kuepuka maafa na kupunguza athari za mafuriko jijini Dar es Salaam.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!