Latest Posts

DC KASESELA AKABIDHIWA OFISI MVOMERO, ATAKA IWE WILAYA YENYE HUDUMA BORA KWA JAMII

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Richard Kasesela, amekabidhiwa rasmi ofisi na kuanza majukumu yake ya kuiongoza Wilaya hiyo na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya,Maulid Hassan Dotto, ambaye kwa sasa amehamishiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Malinyi huku akieleza dhamira ya kuhakikisha Mvomero inakuwa Wilaya yenye huduma bora, zinazowajibika na zinazozingatia mahitaji ya wananchi.

Makabidhiano hayo yamefanyika Oktoba 06, 2026 katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ambapo yanaashiria rasmi kuanza kwa majukumu yake ya kuiongoza Wilaya ya Mvomero.

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Kasesela amesema anahitaji Mvomero iwe Wilaya yenye huduma bora kwa wateja huku akiwataka watumishi kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Amesema atazingatia nidhamu, uwajibikaji, uadilifu na ushirikiano katika kuhakikisha Serikali inatimiza wajibu wake katika kuwahudumia wananchi na wananchi nao watimize wajibu wao. Aidha, Mhe. Kasesela ameeleza kuwa atashirikiana na viongozi pamoja na wananchi kuhakikisha fursa zilizopo zinatumika ipasavyo ili maendeleo yanapatikana.

Awali aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo Maulid Hassan Dotto amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteuwa kuwa msaidizi wake katika nafasi ya Mkuu wa ya Mvomero na sasa Wilaya ya Malinyi. Aidha, amewapongeza na kuwashukuru Viongozi na wananchi wa Wilaya ya Mvomero kwa kumpa ushirikiano katika kipindi chote akiwataka ushirikiano huo kuuendeleza kwa Mkuu mpya wa Wilaya.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Majuka Koila amemshukuru Mhe. Maulid Hassan Dotto kwa uongozi wake uliotukuka katika kipindi alichohudumu akiwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero huku akimtakia kila la heri katika kituo chake kipya cha kazi. Pia, amempongeza Mhe. Richard Kasesela kwa kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mvomero akiahidi kwa niaba ya baraza la madiwani, Menejimenti na watumishi wa Halmashauri hiyo kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Menejimenti, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero Ndg. Paulo Faty amemkaribisha Mhe. Kasesela na kuahidi kumpa ushirikiano na kwamba malengo ya Serikali ya kuwahudumia wananchi yanatimia. Aidha, amemshukuru na kumpongeza Mhe. Maulid Hassan Dotto kwa kuendelea kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Wilaya ya Malinyi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!