Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray, ameitaka jamii kutowaficha watoto wenye mahitaji maalum, bali kuwapa nafasi ya kupata elimu na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii kama ilivyo kwa watoto wengine.
Qwaray, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, ametoa wito huo wilayani Simanjiro wakati akikabidhi vitimwendo saba kwa watoto wenye mahitaji maalum, hususan wenye ulemavu wa viungo, ikiwa ni hatua ya kurahisisha maisha yao ya kila siku.

Aidha, ametoa wito kwa watu wenye uwezo kujitokeza na kuwasaidia watoto na watu wengine wenye mahitaji maalum kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali kulingana na uwezo wao.
Qwaray amesema viti mwendo hivyo pia vitasaidia kupunguza mzigo kwa wazazi na walezi ambao hulazimika kuwabeba watoto wenye ulemavu wanapokwenda shule au kushiriki shughuli nyingine za kijamii.
Kwa upande wao, baadhi ya wazazi walionufaika na msaada huo wamemshukuru Qwaray, wakisema vitimwendo hivyo vitawasaidia kurahisisha maisha ya watoto wao, kuwawezesha kushiriki katika shughuli mbalimbali na kupunguza changamoto ya kuwabeba mgongoni wanapokwenda shule au kushiriki shughuli za kijamii.
