Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limepokea silaha aina ya gobore sitini na nane (68) kutoka kwa wananchi ambao wameitikia wito wa kusalimisha silaha hizo haramu katika kipindi cha msamaha, kabla ya zoezi hilo kuhitimishwa Oktoba 31, 2026.
Akizungumza na vyombo vya habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Almachius Mchunguzi, amesema wananchi wameonesha mwitikio mkubwa kutokana na elimu inayotolewa na Jeshi la Polisi kuhusu umuhimu wa kusalimisha silaha hizo.

Amesema wananchi wamekuwa wakizifikisha wenyewe katika vituo vya Polisi kwa ajili ya kuzisalimisha, hatua ambayo inawapa fursa ya kutekeleza wito huo ndani ya kipindi cha msamaha na kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria baada ya muda huo kumalizika.
Aidha, Kamanda Mchunguzi amewataka wananchi wa Mkoa wa Tanga kuepuka kujihusisha na utengenezaji wa silaha aina ya gobore, akisisitiza kuwa utengenezaji na umiliki wa silaha hizo ni kinyume cha sheria.
Amewataka pia wananchi wenye taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na utengenezaji wa silaha hizo kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa.
