Theophilida Felician Mara.
Chama cha tiba asili na tiba mbadala nchini TAMESOT kimelipongeza na kulishukuru jeshi la Polisi halmashauri ya manispaa ya Musoma mjini kushiriki kikao cha uhamasishaji wa mafunzo ya elimu ya Sayansi shirikishi kilichofanyika ukumbi wa halmashauri ya manispaa ya Musoma mjini mkoani Mara.
Pongezi hizo zimetolewa na katibu mkuu wa TAMESOT Bw Lukas Joseph Mlipu anayeendelea na ziara ya uhamasishaji wa elimu hiyo kwa wataalamu watiba asili mikoa kadhaa ya kanda ya Ziwa ikiwemo Mara.
Hotuba ya kiongozi huyo imefafanua kwamba kitendo cha jeshi la Polisi kuwiwa na kushiriki vyema kikao hicho ni hatua nzuri nayenye kujenga imani na upendo kati ya jeshi hilo na wataalamu watiba asili hivyo ni matumaini yao kuwa huo ni mwelekeo mzuri kwa tasnia ya tiba asili utakaosaidia kupiga hatua na kuyapata maendeleo endelevu.
Hata hivyo ameongeza kuwa wao kama TAMESOT wanathamini pakubwa ushirikiano na utayari wa jeshi la Polisi katika kushiriki juhudi za kuelimisha jamii, kuimarisha usalama wa wananchi na kuendeleza matumizi salama ya tiba asili huku akimshukuru kamanda wa jeshi la Polisi Mara aliyetoa ushirikiano na kuwashirikisha Polisi kata kuhakikisha wanashiriki ziara ya vikao vya kiongozi huyo maeneo yote ya Mkoa wa Mara.

Katibu mkuu Lukas pia ameishukuru ofisi ya Mratibu wa tiba asili na tiba mbadala mkoa Mara aliyewahamasisha waratibu wilaya zote za Mara kuwapa ushirikiano TAMESOT katika zoezi hilo la kuwafikia wataalamu watiba asili.
Amelitaja lengo mahususi la mafunzo hayo ni kuelimisha wataalamu watiba asili na tiba mbadala kupata elimu itakayowawezesha kuelewa umuhimu wa usalama wa mgonjwa, matumizi sahihi ya tiba, utafiti na ushahidi wa kisayansi katika kuboresha huduma zao kwa jamii.
Amehitimisha akiwasisitiza wataalamu watiba asili nchini kuwa huu niwakati mzuri kwao kuungana, kujifunza na kujenga tasnia yenye heshima.
Ziara hiyo ya uhamasishaji inaihusisha mikoa sita ambayo ni Mara, Mwanza, Kagera, Simiyu, Singida na Shinyanga hivyo kiongozi ngozi huyo ametoa wito akiwahimiza waratibu wa TAMESOT na wadau wengine kuendelea kuwahamasisha wataalamu wa tiba asili umuhimu wa mafunzo hayo ambayo yanatarajia kuanza mwezi Novemba 2026.
