Mkazi wa Kijiji cha Mswaki, Wilaya ya Kilindi, Mkoa wa Tanga, Charles Juma, amejitokeza na kusalimisha kwa hiari silaha yake aina ya Gobore baada ya kusikia tangazo la Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Paschal Katambi Patrobas, wakati akizindua Kampeni ya Kitaifa ya Msamaha wa Usalimishaji wa Silaha Haramu.
Charles amesalimisha silaha hiyo katika mkutano wa utoaji elimu kuhusu usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari uliofanyika katika Kijiji cha Mswaki, ambapo baada ya kusikia elimu na ujumbe wa kampeni hiyo, aliamua kufuata nyumbani kwake kuchukua silaha hiyo na kuirejesha katika eneo la mkutano kwa ajili ya kuisalimisha.
Hatua hiyo imekuja baada ya Kikosi Kazi kutoka Kitengo cha Silaha, chini ya Kamisheni ya Upelelezi na Makosa ya Jinai, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, kufika katika eneo hilo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu Kampeni ya Kitaifa ya Msamaha wa Usalimishaji wa Silaha Haramu.
