Kaya 12 katika Kijiji cha Ng’enza, Kata ya Magulilwa, Wilaya ya Iringa, zimeathirika na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali Oktoba 21, 2026, hali iliyosababisha nyumba kuezuliwa mapaa, vyakula kulowa na familia kukosa makazi salama.
Mvua hiyo imeathiri vitongoji vya Lutengelo na Muungano, huku baadhi ya wananchi wakikabiliwa na changamoto za kupata makazi na mahitaji muhimu ya kila siku.
Miongoni mwa walioathirika ni Elizabeth Ngailevanu, mjane mwenye watoto wanne wadogo, ambaye nyumba yake imeezuliwa na upepo na kusababisha vyakula vyake kulowa.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, kupitia katibu wake Yustini Mgao, ametoa msaada wa shilingi milioni 1.5 kwa ajili ya kusaidia kaya 12 zilizoathirika na maafa hayo.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya mbunge, Mgao amewapa pole waathirika na kuwahakikishia kuwa mbunge yupo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu, akisema msaada huo unalenga kuwafariji wananchi na kuwasaidia kukabiliana na changamoto zilizosababishwa na mvua hiyo.
Diwani wa Kata ya Magulilwa, Boaz Mbilinyi, ameishukuru Ofisi ya Mbunge wa Kalenga kwa msaada huo na kutoa wito kwa wadau, taasisi, mashirika na watu wenye uwezo kujitokeza kusaidia familia zilizoathirika, hasa katika kurejesha makazi na kupata mahitaji muhimu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Ng’enza, Amatus Kindole, amesema mvua hiyo imeleta athari kubwa katika vitongoji hivyo, akibainisha kuwa kwa uzoefu wake kijiji hicho hakijawahi kukumbwa na hali kama hiyo kwa kiwango walichokishuhudia.
Naye Elizabeth Ngailevanu ameishukuru Ofisi ya Mbunge wa Kalenga kwa msaada uliotolewa, huku akiiomba jamii na wadau wengine kumsaidia kurejesha nyumba yake ili yeye na watoto wake waweze kupata hifadhi salama.
Hata hivyo Mtendaji wa Kata ya Magulilwa, Merad Mpulule, amesema Serikali inaendelea kufuatilia hali ya wananchi walioathirika na kuwahimiza kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika huku akiwataka wananchi kutoa taarifa mapema kwa viongozi wanapoona viashiria vya hatari, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kuwasaidia waathirika na kulinda maisha pamoja na mali zao.
