Latest Posts

CCT YAITISHA MAOMBI YA TOBA MWAKA 1 BAADA YA MATUKIO YA OKT. 29

Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imetoa wito wa kitaifa kwa makanisa yote wanachama nchini kuungana katika maombi maalum ya toba, rehema, amani na haki, kuelekea kutimiza mwaka mmoja tangu kutokea kwa matukio ya mauaji na umwagaji damu wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025.

Wito huo umetolewa katika taarifa rasmi iliyosainiwa na Mwenyekiti wa CCT, Askofu Dkt. Stanley Hotay ikielekezwa kwa Maaskofu, Viongozi Wakuu, na Wakuu wa Makanisa yote wanachama wa CCT nchini.

Katika taarifa hiyo, CCT imebainisha kuwa ni wajibu wa Kanisa kumwomba Mungu kulirehemu taifa na kuponya majeraha ya matukio yaliyopita, ili kuzuia kujirudia kwa umwagaji damu na kuvunjika kwa amani.

“Wote tunafahamu kuwa ni takribani mwaka mmoja tangu matukio ya mauaji, umwagaji damu na uvunjifu wa amani kutokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025, hivyo kama Kanisa ni wajibu wetu na inafaa tumwombe Bwana, Mungu wetu; Aturehemu na kutusamehe kwa dhambi na makosa wetu kama taifa na kwa kumwaga damu isiyo na hatia katika Taifa”. Imeeleza taarifa hiyo.

Dkt. Hotay ameongeza kuwa maombi hayo yanadhaniwa kuwafariji waliofiwa na kuleta uponyaji kwa waliojeruhiwa, akisisitiza”Tumwombe Mungu atulinde dhidi ya kurudia matukio kama hayo na atujalie amani, haki, umoja na maridhiano ya kweli katika Taifa letu la Tanzania”.

Akinukuu Neno la Mungu kutoka 2 Mambo ya Nyakati 7:14, Dkt. Hotay ameitaka jamii kujinyenyekesha mbele ya Mungu, kuacha njia mbaya ili Mungu aisikie nchi na kuiponya.

Mbali na maombi ya amani na haki, taarifa hiyo ya CCT imegusia pia utabiri wa hali ya hewa uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) unaoonesha uwezekano wa mvua kubwa na maafa, ikihimiza waumini kuomba Mungu kuepusha mafuriko, uharibifu wa mali, mazao, miundombinu, magonjwa, na kupoteza maisha.

Dr. Hotay ameeleza kuwa waumini wanapaswa kuomba ili Mungu ajaalie mvua za wastani zitakazosaidia kilimo na ustawi wa taifa, pamoja na kupewa hekima ya kuchukua tahadhari zinazostahili.

Akinukuu Maandiko Matakatifu ya Isaya 43:2 na Zaburi 46:1, Dr. Hotay amesema, “Kitabu Cha Zaburi 46:1 kinatukumbusha kuwa: ‘Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.’ Kwa hiyo, sisi kama Kanisa na viongozi tuendelee kumtegemea Mungu kwa imani, hata katika nyakati hizi za matetesho ya Maafa na majaribu ya amani na haki katika Taifa Letu, huku tukiendelea kutenda kwa upendo na kujenga amani katika jamii zetu”.

CCT imewataka viongozi wote wa makanisa wanachama kuongoza maombi hayo katika ibada, mikutano ya maombi, na vikundi vya waumini kote nchini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!