Mkutano wa 11 wa Kitaifa wa Kilimo Misitu nchini Tanzania unatarajiwa kufanyika kuanzia Oktoba 19 hadi 21, 2026, katika Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Misitu kilichopo Bweri, Musoma, mkoani Mara, ukiwa na lengo la kufungua fursa za uwekezaji wa kijani unaoongozwa na vijana pamoja na kuimarisha mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Musoma, Meneja wa Vi Agroforestry nchini, Martha Olotu alisema mkutano huo utawakutanisha wawakilishi wa serikali, vijana, wakulima, wafanyabiashara, taasisi za fedha, watafiti na wadau wa maendeleo ili kujadili fursa za uwekezaji na kuimarisha ushirikiano katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo misitu.
Alisema mkutano huo wa kitaifa unalenga kubaini fursa za uwekezaji na biashara zinazoweza kutekelezeka katika sekta hiyo, huku ukichangia kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula na maendeleo endelevu vijijini.

Kwa mujibu wa Olotu, mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo “Kilimo Misitu kwa Ajili ya Vijana na Uwekezaji wa Kijani,” unalenga kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu kama wakulima, wajasiriamali, wabunifu na viongozi katika kuijenga Tanzania yenye uchumi wa kijani unaostahimili changamoto za kimazingira.
“Majadiliano yatajikita katika upatikanaji wa mbegu na miche bora, uzalishaji endelevu, usindikaji, upatikanaji wa masoko, maendeleo ya biashara na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya uwekezaji wa kijani, kwa lengo la kuifanya sekta ya kilimo misitu kuwa chanzo cha biashara endelevu na ajira zenye staha,” alisema.

Olotu alisema mkutano huo unafanyika wakati Tanzania ikiendelea kutekeleza dhamira yake ya kuhifadhi mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha usimamizi endelevu wa ardhi.
Alieleza kuwa Programu ya Mageuzi ya Usimamizi wa Mazingira kuelekea Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 inalenga kuunga mkono utekelezaji wa dira hiyo, ikiwamo azma ya kupanda miti bilioni mbili kila mwaka, huku Serikali ikiwa na lengo la kupanda miti bilioni 10 ifikapo mwaka 2030.
“Kilimo misitu kinaweza kugeuza malengo haya kuwa matokeo halisi kwa kuboresha rutuba ya udongo, kuimarisha upatikanaji wa maji, kurejesha bioanuwai, kuongeza kipato cha wananchi wa vijijini na kujenga mifumo ya chakula inayostahimili changamoto mbalimbali.

“Matokeo haya yanaendana pia na vipaumbele vya Afrika na dunia kwa ujumla katika kutafuta suluhisho zinazotekelezeka na zinazoongozwa na jamii husika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa ardhi na ukosefu wa ajira kwa vijana,” alisema.
Alisisitiza kuwa ili kufikia manufaa hayo, ni muhimu kuachana na mtazamo wa kampeni za muda mfupi za upandaji miti na kuelekea katika mifumo endelevu ya uzalishaji inayohakikisha miti inastawi, inazalisha thamani ya kiuchumi na kusaidia kuimarisha mashamba, biashara na mazingira kwa muda mrefu.
Alisema vijana wana fursa ya kuanzisha na kuendeleza biashara zinazohusiana na ukusanyaji wa mbegu, uanzishaji wa vitalu vya miche, upandaji na utunzaji wa miti, utoaji wa huduma za kitaalamu, matumizi ya teknolojia za kidijitali, usindikaji na uuzaji wa mazao.
Hata hivyo, alisema ili vijana waweze kutumia fursa hizo kikamilifu, wanahitaji ujuzi wa vitendo, upatikanaji salama wa ardhi, mitaji, huduma za kuwaendeleza kibiashara, huduma za ugani pamoja na masoko ya uhakika.
Olotu alisema Mkakati wa Taifa wa Kilimo Misitu Awamu ya Pili (2024–2031) unaweka msingi wa kuratibu utekelezaji wa shughuli za sekta hiyo, akibainisha kuwa kipaumbele cha sasa ni kuhakikisha mkakati huo unatafsiriwa katika bajeti, huduma na uwekezaji katika ngazi za kitaifa na za maeneo husika.