Latest Posts

PROF. KITILA AZIKARIBISHA KAMPUNI ZA UHOLANZI KUWEKEZA TANZANIA KWENYE MADINI, KILIMO NA BANDARI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo, amezikaribisha kampuni na wawekezaji kutoka nchini Uholanzi na Umoja wa Ulaya (EU) kuja kuwekeza nchini Tanzania katika maeneo ya kimkakati ya madini, kilimo, na ugavi wa bandari badala ya kuishia kufanya biashara ya kawaida tu.

Prof. Mkumbo ameyasema hayo tarehe 5 Oktoba 2026 mjini The Hague, Uholanzi, wakati wa Mkutano wa Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na EU, akieleza kuwa nafasi ya kimkakati ya Tanzania kijiografia, pamoja na miundombinu na masoko yanayozunguka nchi, vinaifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha uzalishaji, biashara na usambazaji wa bidhaa katika masoko ya Afrika na kwingineko.

Ameeleza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za madini ikiwemo dhahabu, kinywe, nikeli, shaba, na madini adimu yanayohitajika duniani kwa ajili ya nishati safi. Amesisitiza kuwa lengo la Serikali si kuuza madini ghafi nje ya nchi, bali ni kuongeza thamani, kuchakata, na kuyaunganisha katika mnyororo wa thamani wa kimataifa.

“Lengo letu si kuuza tu madini kama malighafi ghafi. Tunataka kukuza maendeleo ya madini yenye uwajibikaji, uongezaji thamani, uchakataji, viwanda na kuunganishwa kwenye mnyororo wa thamani wa kimataifa… Kwa upande wetu, mustakabali wa sekta ya madini lazima uwe kuhusu uongezaji thamani, uendelevu na ustawi wa pamoja”, ameeleza.

Katika sekta ya kilimo, Waziri Mkumbo alibainisha kuwa Tanzania inalenga kutoka kwenye uzalishaji wa mazao ya msingi pekee na kuelekea kwenye uchakataji, ufungashaji, na uuzaji wa bidhaa zenye thamani kubwa. Ameongeza kuwa sekta ya kilimo na lojistiki lazima zikue pamoja kwani bila miundombinu bora ya hifadhi, ubaridi na usafirishaji, thamani kubwa ya mazao ya wakulima inapotea.

Kuhusu lojistiki ya bandari na uunganishaji wa kikanda, Prof. Mkumbo ameeleza kuwa Bandari ya Dar es Salaam inahudumia takriban asilimia 95 ya biashara ya kimataifa ya Tanzania pamoja na nchi jirani zisizokuwa na bahari kama Zambia, Malawi, DRC, Burundi, Rwanda, Uganda, na Zimbabwe. Amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuwekeza kwenye maboresho ya miundombinu ya bandari ikiwemo mradi wa Dar es Salaam Marine Gateway na Bandari ya Kina Kirefu ya Bagamoyo.

Prof. Mkumbo ameeleza pia kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, ikiwamo kurahisisha huduma kwa wawekezaji na kuweka mazingira yanayowezesha sekta binafsi kuwa injini muhimu ya maendeleo ya Taifa.

Mkutano huo ni sehemu ya ziara ya uhamasishaji wa uwekezaji barani Ulaya, iliyoanza Helsinki, Finland tarehe 28 Septemba 2026, na kuendelea nchini Italia kabla ya kufika Uholanzi. Ziara hiyo pia ni sehemu ya maandalizi kuelekea Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, linalotarajiwa kufanyika Dar es Salaam mwaka 2027.

 

Kupitia ziara hiyo, Tanzania inalenga kuimarisha mahusiano na jumuiya ya wafanyabiashara wa Ulaya, kuvutia mitaji mipya na teknolojia, pamoja na kubadilisha majadiliano ya uwekezaji kuwa miradi halisi inayotekelezwa nchini.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!