Latest Posts

SAMIA MGENI RASMI KILELE MAADHIMISHO MIAKA 70 YA TAASISI ZA KIRAIA OKTOBA 29

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi ametangaza kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Ofisi ya Msajili wa Taasisi za Kiraia inatarajia kuadhimisha miaka 70 ya usajili, usimamizi, na udhibiti wa taasisi hizo nchini kuanzia tarehe 27 hadi 29 Oktoba, 2026, katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Oktoba 13, 2026 jijini Dar es Salaam, Katambi ameeleza kuwa usajili wa taasisi hizo unaofanyika chini ya Sheria ya Usajili wa Jumuiya za Kiraia (Sura namba 337) una lengo kuu la kulinda na kudumisha amani na usalama wa nchi, huku ikijumuisha taasisi za kidini, kimila, kibiashara, na kijamii.

Katambi amebainisha kuwa Mgeni Rasmi katika siku ya kilele cha maadhimisho hayo tarehe 29 Oktoba 2026 anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Katika siku hiyo ya tarehe 29 na siku ya kilele chake tarehe 27 na kilele chake tarehe 29, Mgeni rasmi wa shughuli hii anatarajiwa kuwa mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania… Kauli mbiu ya maadhimisho haya ya miaka 70 ya usajili, usimamizi, udhibiti na uendeshaji wa taasisi za kiraia inasema: ‘Jumuiya za kiraia ni msingi wa umoja, mshikamano na maendeleo ya taifa’

Ameongeza kuwa maadhimisho hayo yatatoa fursa na jukwaa maalum la kuimarisha amani na usalama, kuboresha ushirikiano wa kimkakati kati ya serikali na taasisi za kiraia, pamoja na kukusanya maoni, ushauri, na mijadala ya kuboresha sera, sheria, na mifumo ya utendaji wa taasisi hizo ili kuwahudumia Watanzania kwa ufasaha.

“Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia ofisi ya msajili wa asasi za kiraia au taasisi za kiraia inayo dhamana ya usajili, usimamizi lakini pia udhibiti wa taasisi za kiraia. Na katika wajibu huo upo kwa mujibu wa sheria sura namba 337… Wizara ya Mambo ya Ndani tangu kuanza kwa jukumu hilo chini ya kitengo husika mpaka sasa mwaka 2026 tunaadhimisha miaka 70 ya usajili wa taasisi za kiraia”

Maadhimisho hayo yatawakutanisha viongozi wa taasisi za dini, viongozi wa kijamii na kimila, wanazuoni, wageni kutoka ndani na nje ya nchi, viongozi wa serikali, pamoja na wawakilishi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na benki za biashara.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!