Taifa la Uingereza limeionya rasmi Israel kuwa itawafukuza wanadiplomasia wake 27 kutoka London ikiwa Tel Aviv itatekeleza agizo la kufunga Ofisi ya Ubalozi Mdogo wa Uingereza (Consulate General) iliyopo Mashariki mwa Jerusalem.
Onyo hilo limewasilishwa na Balozi wa Uingereza nchini Israel, Simon Walters, leo Octoba 06,2026 wakati akisisitiza kuwa London itaondoa mwanadiplomasia mmoja wa Israel kwa kila afisa mmoja wa Uingereza ambaye vibali vyake vitafutwa na serikali ya Israel. ilifuatia mipango ya Israeli ya kujenga nyumba mpya 1,200 katika eneo linalokaliwa, na kusababisha lawama kubwa za kimataifa, kwani makazi yote katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa
Baadhi ya wachambuzi wa mambo ya nje ulimwenguni wanaeleza kuwa mvutano huu ni hatua mbaya zaidi ya kidiplomasia kuwahi kushuhudiwa kati ya mataifa haya mawili tangu kuundwa kwa taifa la Israel.
Hata hivyo ripoti mbalimbali zikiwemo zilizochapishwa na mtandao wa habari wa Israel, Ynet, na shirika la habari la Reuters, zinaeleza kuwa mzozo huu ulianza mwezi uliopita baada ya serikali ya chama cha Labour nchini Uingereza kuweka vikwazo vikali vya kiuchumi na marufuku ya biashara dhidi ya bidhaa zinazotoka kwenye makazi haramu ya walowezi wa Kiisrael katika Ukingo wa Magharibi.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Sa’ar, analaani hatua hiyo akiiita kuwa ni “upotoshaji wa kimaadili” na kulipiza kisasi kwa kuamuru ubalozi mdogo wa Uingereza uliopo Sheikh Jarrah, Mashariki mwa Jerusalem, ufungwe ifikapo tarehe 8 Oktoba 2026, huku Israel ikiwa tayali imewapa wanadiplomasia wa Uingereza waliopo hapo, pamoja na wale wanaoratibu misaada ya Gaza na waliopo Ramallah, muda wa siku 30 tu kuondoka nchini humo.
Licha ya juhudi za siri za dakika za mwisho zilizofanywa na Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Uingereza, Jonathan Powell, aliyesafiri hadi Jerusalem kujaribu kuishawishi Israel isifunge ubalozi huo, inaelezwa kuwa mazungumzo hayo yamegonga mwamba bila kufikia muafaka.
Wakati huohuo, vyanzo vya kidiplomasia kutoka Israel vimeiambia The Jerusalem Post kuwa nchi hiyo haitatikisika kwa vitisho vya Uingereza na kwamba hatua yoyote itakayochukuliwa dhidi ya Israel itajibiwa kwa kiwango kilekile. Ikiwa Uingereza itatekeleza tishio lake la kufukuza maafisa 27, ubalozi wa Israel mjini London utapata pigo kubwa la kiutendaji.